Shein asema uchaguzi utarudiwa Zanzibar

Magufuli Haki miliki ya picha Statehouse Zanzibar
Image caption Rais wa muungano wa Tanzania John Magufuli alihudhuria maadhimisho hayo

Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein amesisitiza kwamba uchaguzi visiwani humo utarudiwa licha ya Chama cha Wananchi (CUF) kupinga wazo hilo.

Akihutubu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi, Dkt Shein amesisitiza kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliyafuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka jana.

Hata hivyo, amesema mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mzozo huo wa Zanzibar bado inaendelea na taarifa ya pamoja itatolewa baada ya mazungumzo kukamilika.

“Tume ya Uchaguzi iliufuta uchaguzi wa Zanzibar tarehe 28 Oktoba, 2015, baada ya kubainika kutokea kwa kasoro kadhaa kama zilivyoelezwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,” amesema.

“Nawaomba wananchi waendelee kuishi kwa amani na kupendana huku tukisubiri Tume ya Uchaguzi Zanzibar itangaze tarehe nyengine ya kurudia uchaguzi.”

Haki miliki ya picha Statehouse Zanzibar
Image caption Viongozi wa chama cha CUF walisusia sherehe hizo

Kiongozi wa chama cha CUF Maalim Seif akiwahutubia wanahabari jijini Dar es Salaam alikuwa amesema chama chake hakitakubali kurudiwa kwa uchaguzi.

Alionya kuwa hatua kama hiyo inaweza kuzua vurugu visiwani na kumuomba Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli aingilie kati.

Awali, chama cha CCM kilikuwa kimewahimiza wafuasi wake visiwani humo wajiandae kwa marudio ya uchaguzi.

Siku ya Mapinduzi hutumiwa kuadhimisha miaka 52 tangu kufanyika kwa Mapinduzi yaliyoondoa utawala wa Sultani tarehe 12 Januari 1964.