Nakala za bajeti zatoweka Nigeria

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Nakala za bajeti zatoweka Nigeria

Mamia ya nakala za bajeti rasmi ya serikali ya Nigeria ya mwaka wa 2016, zimetoweka kutoka bunge la nchi hiyo.

Haya ni kwa mujibu wa mbunge mmoja aliyezungumza na BBC na ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Bunge la Senate lilishindwa kuanza kujadili mapendekezo ya bajeti hiyo kwa sababu ya nyaraka hizo kupotea.

Hali hiyo sasa huenda ikahujumu uchumi wa taifa hilo ambao umeathirika pakubwa kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta.

Rais Muhammadu Buhari aliwasilisha nyaraka hizo kwa mabunge yote mawili mwezi uliopita.

Serikali ya nchi hiyo ilikuwa imependekeza nyogesa ya asilimia ishirini ya matumizi ya serikali, na kuifadhili nyongesa hiyo kupitia mikopo zaidi huku bei ya mafuta ikiendelea kushuka.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wabunge wa upinzani wamegadhabishwa na kutoweka kwa nyaraka hizo na kudai kuwa serikali ilihusika.

Buhari ambaye alitwaa madaraka ya nchi hiyo Mei mwaka uliopita, alihaidi kuimarisha ukusanyaji wa ushuru na kuwa serikali itawekeza zaidi katika secta nyingine kama vile uchimbaji wa madini na kilimo ili kubuni nafasi zaidi za kazi.

Rais wa bunge la Senate Bukola Saraki alifanya mazungumzo ya faragha na rais Buhari siku ya Jumanne, lakini haijabainika ikiwa suala hilo la kutoweka kwa nakala za bajeti lilijadiliwa.

BBC imepata ripoti kuwa nakala zilizowasilishwa kwenye bunge la nchi hiyo hazikupotea na zitasambazwa leo kwa wabunge.

Wabunge wa upinzani wamegadhabishwa na kutoweka kwa nyaraka hizo na kudai kuwa serikali ilihusika.

Lakini msemaji wa rais Buhari Garba Shehu amekanusha madai hayo na kusema kuwa pindi ofisi ya rais ikiwasilisha makadirio ya bajeti kwa bunge, nakala hizo sio mali ya ofisi ya rais tena.

Mabunge hayo mawili yanatarajiwa kuchukua muda wa miezi miwili kujadili bajeti hiyo inayokisiwa kugharimu dola bilioni 31 za Marekani.