Mahakimu wanane wafutwa kazi Kenya

Rao Haki miliki ya picha JMVB
Image caption Bodi hiyo imependekezwa kuundwe mamlaka ya kupokea malalamiko dhidi ya maafisa wa mahakama

Mahakimu wanane nchini Kenya wamefutwa kazi baada ya kupatikana na makosa ya kujihusisha na ufisadi na kutumia vibaya mamlaka.

Mahakimu hao wamefutwa kazi na Tume ya Kuchunguza Majaji na Mahakimu ambayo imekuwa ikiwachunguza wahudumu wa idara ya mahakama waliokuwa kazini kabla ya Agosti 2010, katiba ya sasa ilipoidhinishwa.

Walikuwa miongoni mwa mahakimu 36 waliochunguzwa katika mkumbo wa sasa.

Mwenyekiti wa bodi hiyo Sharad Rao amesema baadhi ya mahakimu hao wanane walijihusisha na ufisadi na wengine hawakuwa na uwezo wa kufanya uamuzi mwafaka.

Katika kisa kimoja, bodi hiyo inasema hakimu mmoja aligunduliwa kuwa na matatizo katika matumizi ya pesa na hata kushindwa kulipa madeni.

"Jambo kama hili ni la kutia wasiwasi likitokea kwa afisa wa mahakama. Anatakiwa kuwa mtu wa kuwajibika kwa kulipa madeni yake kwa wakati. Afisa wa mahakama, asiyesimamia fedha zake vyema, anaweza kuhongwa kwa urahisi,” taarifa ya bodi hiyo inasema.

Bodi, baada ya kuchunguza mtindo wa maisha wa mahakimu na kutathmini utendakazi wao, imesema imeingiwa na shaka kuhusu uwezo wa mahakimu kufanya kazi yao.

Tume hiyo inapendekeza kubuniwe mamlaka huru ya kupokea malalamiko dhidi ya maafisa wa mahakama.

Aidha, inapendekeza idara ya mahakama ishirikiane na vyuo vikuu kuweka mpango wa kutoa mafunzo zaidi kwa maafisa wanaohudumu katika idara ya mahakama.

Bodi hiyo inatarajiwa kumaliza kazi yake kufikia mwisho wa Machi 2016.