Sierra Leone yaripoti kisa cha ebola

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sierra Leone yaripoti kisa chengine cha ebola

Siku moja tu baada ya shirika la afya duniani WHO kutangaza kumalizika kwa Ebola huko Afrika magharibi ,maafisa wa Sierra Leone wamesema wanachunguza kifo kimoja cha mgonjwa ambacho sasa kimebainika kimetokana na Ebola.

Ebola imesababisha vifo vya zaidi ya watu elfu 11 katika mataifa ya Guinea, Liberia na Sierra Leone tangu kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa huo miaka miwili iliyopita.

Taifa hilo lilitangazwa kuangamiza Ebola mnamo mwezi Novemba, na eneo hilo kwa jumla lilitangazwa lisilo na ugonjwa huo baada ya Liberia kutangazwa kuumaliza ugonjwa huo siku ya Alhamisi.

Vipimo vilivyofanyiwa mtu huyo aliyefariki kutokana na ugonjwa huo kaskazini mwa Sierra Leone vilithibitisha hilo,msemaji wa kituo kimoja cha kupima ugonjwa huyo aliiambia BBC.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mtu aliyefariki kutokana na ugonjwa wa ebola

Shirika la afya duniani WHO limeonya ,hatahivyo kwamba linatarajia hisia kali kutolewa.

Kifo hicho kilitokea mapema wiki hii.Shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba mwathiriwa ni mwanafunzi wa miaka 22.

Shirika hilo pia limesema kwamba lina habari kutoka kwa shirika moja la hisani kwamba mgonjwa huyo alitibiwa kama mgonjwa wa kuingia na kutoka.