Utata kuhusu mdahalo wa urais Uganda

Museveni Haki miliki ya picha AP
Image caption Bado haijulikani iwapo Rais Museveni atashiriki

Wagombea urais nchini Uganda leo wanatarajiwa kushiriki katika mdahalo wa kwanza kabisa wa wagombea urais runingani nchini humo.

Mdahalo huo umepangiwa kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Kampala kuanzia saa moja jioni saa za Afrika Mashariki.

Hata hivyo, bado kuna shaka kuhusu iwapo wagombea wote wanane watashiriki kwenye mdahalo huo.

Rais Yoweri Museveni, ambaye ameongoza taifa hilo kwa miaka 30 sasa, alikuwa amedokeza kwamba hatashiriki mdahalo huo uamuzi uliomfanya mgombea wa upinzani Kizza Besigye kusema naye pia angesusia.

Lakini Alhamisi, Dkt Besigye, anayetumia chama cha Forum for Democratic Change, alisema atashiriki akisema alikutana na Jaji James Ogoola ambaye alimhakikishia kwamba Bw Museveni angeshiriki.

Msemaji wa serikali Ofwono Opondo alikuwa awali amesema kiongozi huyo hangehudhuria.

Image caption Dkt Besigye alikuwa ametishia kutoshiriki Bw Museveni akisusia

Alisema rais anaonelea heri kutumia muda huo akitembelea wapiga kura vijijini na kuwaomba wampigie kura.

Wengine wanaowania urais kwenye uchaguzi utakaofanyika Februari 18 ni waziri mkuu wa zamani Amama Mbabazi, Prof Venansius Baryamureeba, Bi Maureen Kyalya, Dkt Abed Bwanika, Bw Joseph Mabirizi na Jenerali Benon Biraaro.