Akamatwa akihusishwa na wanamgambo wa IS

Image caption Watu 130 walipoteza maisha kwenye mashambulizi ya jijini Paris

Polisi nchini Morocco wamemkamata raia wa ubelgiji mwenye asili ya Morocco, wakisema anahusishwa na kundi la Islamic state na ana uhusiano wa moja kwa moja na washambuliaji waliowaua watu 130 jijini Paris Ufaransa miezi miwili iliyopita, Wizara ya mambo ya ndani ya Morocco imeeleza.

Mtu huyo alisafiri mpaka Syria na mmoja wa waliojitoa muhanga jijini Paris, ambapo alipatiwa mafunzo ya kijeshi na kujenga uhusiano na makamanda wa IS akiwemo aliyepanga mashambulizi ya Paris na wengine waliotishia mashambulizi nchini Ufaransa na Ubelgiji, wizara hiyo imeeleza kwenye taarifa yake.

Taarifa ya wizara hiyo imemtambua mshukiwa kwa majina ya ufupisho ya J.A na haikuelezwa kuhusu uhusiano wake washambuliaji wa Paris.

Mwendesha mashtaka nchini Ubelgiji, Eric Van der Sypt aliliambia shirika la habari la AP kuwa mshukiwa huyo jina lake ni Gelel Attar, mwenye uraia pacha wa Ubelgiji na Morocco, alishatuhumiwa kujihusisha na kundi la kigaidi hapo awali.

Wanamgambo wa kiislamu waliotekeleza shambulizi kwenye tamasha la jijini Paris na migahawa mnamo tarehe 13 mwezi Novemba wengi wao wana asili ya Morocco na Ubelgiji.

Mtu huyo ambaye alikamatwa siku ya ijumaa mjini Mohammedia karibu na Casablanca baada ya kusafiri kupita Uturuki, Ujerumani, Uholanzi na Ubelgiji hivi sasa anachunguzwa.