Kenya yatafuta manusura wa shambulio Somalia

majeruhi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Majeruhi wanaendelea kupokelewa uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi

Majeshi ya Kenya yameendelea na operesheni ya kuwasatafuta manusura kutoka kwa shambulio la wapiganaji wa al-Shabab katika kambi ya jeshi ya el-Ade nchini Somalia.

Operesheni hiyo inaendelea huku wanajeshi zaidi waliojeruhiwa wakati wa shambulio hilo la Ijumaa wakiendelea kupokelewa uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi. Jumla ya wanajeshi 16 walisafirishwa hadi Nairobi leo, wengi wakiwa wameathirika na mshtuko.

Kenya ina takriban wanajeshi 4,000 ambao ni sehemu ya kikosi cha wanajeshi 22,000 wa Muungano wa Afrika nchini Somalia.

Wanajeshi hao wamekuwa wakisaidia serikali ya nchi hiyo dhidi ya wapiganaji wa al-Shabab.

Kundi la al-Shabab limesema liliwaua wanajeshi zaidi ya 60 na kuwateka nyara wengine.

Serikali imesema idadi hiyo iliyotolewa na al-Shabab ni propaganda na si ya kweli. Hata hivyo, serikali bado haijatoa idadi rasmi ya wanajeshi waliouawa au kujeruhiwa wakati wa shambulio hilo.

Mkuu wa majeshi ya Kenya Samson Mwathethe Jumapili alisema wapiganaji hao wanawatumia baadhi ya wanajeshi waliowateka nyara kama kinga dhidi ya mashambulizi.