Rais wa Senegal kupunguza miaka ofisini

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Macky Sall aliahidi kupunguza muhula wake wakati wa kampeni zake za uchaguzi mwaka 2012

Rais wa Senegal Macky Sall amependekeza kupunguza miaka ya muhula wake mwenyewe ofisini kwa miaka miwili.

Rais Macky Sall aliahidi kufanya hivyo wakati wa kampeni zake za uchaguzi mwaka 2012. Wapinzani wake wamekuwa wakitoa wito atimize ahadi hiyo.

Kubadilisha miaka ya kuongoza kutoka saba hadi tano ni moja ya mapendekezo ya madadiliko kwa katiba ambayo itapigiwa kura.

Kwa kawaida nchini Senegal muhula wa rais kuhudumu madaraka huwa ni miaka saba. Sasa rais aliyeko madarakani, anataka kipindi hiki kupunguzwa kwa miaka miwili ili mhula uwe na miaka mitano.

Haki miliki ya picha
Image caption Anapunguza miaka licha ya marais kadha wa Afrika kubadilisha katiba na kujiongezea mihula yao madarakani.

Kufanya hivi, rais Macky Sall anapendekeza kuhitimisha mhula wake wa kwanza madarakani baada ya miaka mitano.

Kisha anatarajiwa kugombea kiti cha urais mwaka 2017 badala ya mwaka 2019. Lakini kabla ya hapo, raia wa Senegal ni sharti wapige kura ya maoni kufanyia katiba marekebisho vipengee kadhaa, ikiwemo muhula wa rais madarakani.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizochapishwa kutoka ofisi yake, rais ataruhusiwa tu kikatiba kuhudumu madarakani kwa mihula miwili yenye kipindi cha miaka mitano. Pia umri unaohitajika kwa mtu kugombea urais utafanyiwa marekebisho.

Licha hilo marais kadha wa Afrika wamefanya kinyume kwa kubadilisha na kujiongezea mihula yao madarakani.