Mkuu wa tuzo za Oscars akiri tatizo

Isaacs Haki miliki ya picha AP
Image caption Boone Isaacs amesema mabadiliko yanahitajika katika jopo la wanaotoa tuzo za Oscars

Mkuu wa shindano la Oscars Cheryl Boone Isaacs amechukua hatua kuhusiana na tuhuma dhidi ya wajumbe wa shindano hilo, baada ya Spike Lee na Jada Pinkett Smith kukataa kushiriki kwasababu ya uteuzi wa wanaowania tuzo hilo ambapo Wazungu wengi ndio walioteuliwa.

Boone Isaacs alisifu "kazi nzuri " ya uteuzi lakini akasema ''alikatishwa tamaa'' kwa kuwa uteuzi huo ulikosa ''mchanganyiko wa watu wa tabaka mbali mbali'. Lee alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram ''hawezi kuunga mkono" shindano la tuzo za "Wazungu" pekee.

Jada Pinkett Smith amesema kwenye mkanda wake wa video uliotumwa kwenye Facebook kwamba hatahudhuria sherehe za utoaji tuzo Februari 28.

Boone Isaacs aliongeza kuwa "hatua zinazofaa" zinachukuliwaa, akisema: "siku zijazo na wiki tutafanya tathmini ya ajira za watu wetu ili kuwezesha ushirikishi unaohitajika wa watu wa tabaka mbali mbali katika mashindano yajayo ya mwaka 2016 na miaka zaidi ya mbeleni."

Wajumbe wa Oscars, wanatoka katika sekta ya filamu ambao huwateua walioteuliwa kwa mashindano ya tuzo la Oscars kila mwaka "haya ni mazungumzo magumu, lakini ya muhimu, na ni wakati wa mabadiliko makubwa,"alisema. "Kama wengi mnavyofahamu, tumetekeleza mabadiliko kwa ajili ya kushirikisha wajumbe kutoka tabaka mbali mbali kwa miaka minne iliopita... Lakini mabadiliko haya hayaji kwa haraka kama ambavyo tungelipenda. Tunahitaji kufanya juhudi zaidi, nzuri na za haraka zaidi."

Haki miliki ya picha AP
Image caption Jada Pinket (wa pili kulia), amesema hatahudhuria sherehe ya kutangaza washindi wa Oscars

Alisema hatua hiii "haikutarajiwa" katika mashindano haya, na kwamba miaka ya 60 na 70 wajumbe vijana waliajiriwa na kwamba malengo ya sasa yanakaribia kukamilika : " kuzingatia jinsia,rangi, jamii na mtizamo wa kimapenzi ".

Boone Isaacs pia alijaribu kufanya onyesho la tarehe 28 Februari kuwa la watu wa matabaka mbali mbali zaidi, akimfanya msanii mweusi wa vichekesho Chris Rock kuwa mwongozaji wa onyesho hilo.

Huu ni mwaka wa wapili katika mzozo huo ambapo kumekua na miito ya kususia, iliyozushwa na orodha ya walioteuliwa kushiriki onyesho la Oscars kuwa na wazungu zaidi.