Washukiwa wanne wa ugaidi wauawa Kenya

Marwa
Image caption Bw Marwa amesema washukiwa wawili wamefanikiwa kutoroka

Polisi nchini Kenya wamewapiga risasi na kuwaua washukiwa wanne wa ugaidi katika mji wa Malindi eneo la Pwani.

Mmoja wa washukiwa hao amekuwa akitafutwa na polisi nchini Kenya kwa kushukiwa kuhusika kwenye shambulizi lililoendeshwa katika chuo kikuu cha Garisa mwezi Aprili mwaka 2015.

Suleiman Mohammed Awadh, aliuawa pamoja na wenzake wakati polisi walifanya uvamizi mapema leo asubuhi kwenye nyumba moja ya mjini Malindi.

Kamishna wa jimbo la Pwani Nelson Marwa ameambia wanahabari kwamba wanne hao waliwashambulia wa polisi kwa guruneti na risasi kabla ya kuzidiwa nguvu na kuuawa.

Amesema polisi walipata silaha, ramani ya Malindi inayoonyesha maeneo ambayo walilenga kushambulia na barua iliyokuwa imeandikiwa wafadhili wa al-Shabab kuomba pesa, nguo na chakula.

Washukiwa wengine wawili wametoroka wakiwa na majeraha ya risasi, Bw Marwa amesema.