Kenya:Alshabaab walilipua bomu kubwa kambini

Image caption Jenerali Samson Mwathethe

Utata unaoendelea kugubika idadi ya wanajeshi waliouawa siku ya ijumaa wakati wapiganaji wa Alshabaab walipovamia kambi ya wanajeshi wa AMISOM kusini mwa Somalia haujatatuliwa.

Mkuu wa majeshi nchini Jenerali Samson Mwathethe ameuambia mkutano wa wanahabari mjini Nairobi kwamba mamlaka ya jeshi itatoa takwimu za shambulio hilo baada ya kamati aliyoiteua kuchunguza shambuliizi hilo kufanikisha kazi yake.

Jenerali huyo pia amesema kuwa bomu lililotumika na wapiganaji hao ni mara tatu kwa ukubwa wa lile lililotumika katika ubalozi wa Marekani jijini nairobi mwaka 1998 ambalo liliangusha jumba la ghorofa 10.

Kuna wasiwasi nchini Kenya hususan miongoni mwa jamaa na marafiki kuhusu wapendwa wao baada ya serikali kushindwa kutoa idadi ya wanajeshi ambao huenda waliaga dunia,huku wapiganaji wa Alshabaab wakidai kuwaua zaidi ya wanajeshi100.