Mkesha wa wanajeshi wa Kenya waliouawa Somalia

Jeshi
Image caption Idadi kamili ya wanajeshi waliouawa bado haijajulikana

Wanaharakati pamoja na raia wamekusanyika eneo la Freedom Corner, Nairobi kwa mkesha wa kuwakumbuka wanajeshi wa Kenya waliouawa katika shambulio la al-Shabab Somalia.

Wanaharakati hao wanasema Serikali imewasahau wanajeshi hao na jamaa zao.

Wanaoshiriki kwenye mkesha huo wamepanga bendera na mifano ya kofia za wanajeshi. Mishumaa itawashwa usiku kucha.

Idadi ya wanajeshi waliouawa au kujeruhiwa baada ya al-Shabab kushambulia kambi ya el-Ade Ijumaa iliyopita bado haijulikani.

Mkuu wa majeshi ya Kenya Jenerali Samson Mwathethe amesema bado ni mapema kujua idadi hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta, ambaye amekuwa eneo la Pwani kwa karibu mwezi mmoja sasa ametangaza kwamba atarejea Nairobi na kesho anatarajiwa kuzuru hospitali ya wanajeshi ya Forces Memorial kesho kutembelea wanajeshi waliojeruhiwa.

Baadaye, ataungana na jamaa na marafiki kwa sherehe ya kuwakumbuka wanajeshi walioshambuliwa.