Kesi dhidi ya kamanda wa LRA yaendelea ICC

Image caption Dominic Ongwen

Mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC imeanza majadiliano kuhusu iwapo kuna ushahidi wa kutosha wa kumshtaki aliyekuwa kamanda wa kundi la wapiganaji wa Lord's Resistance Army (LRA) nchini Uganda.

Dominic Ong'wen anakabiliwa na mashtaka 67 ya uhalifu dhidi ya binadamu pamoja na yale ya kivita kaskazini mwa Uganda yaliotekelezwa kati ya 2002 na 2005.

Kamanda wa LRA Dominic Ong'wen ameielezea mahakama hiyo kwamba kusikizwa kwa kesi hiyo ni kupoteza mda akidai kuwa mambo mengi yaliodaiwa si ya ukweli.

Image caption Dominic Ongwen

Amesema kuwa aliyasoma na kuyaelewa mashtaka hayo dhidi yake.

Ongwen ambaye alitekwa nyara na kufanywa mwanajeshi na LRA akiwa na umri wa miaka 10, alikamatwa katika taifa la Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR mwezi Januari uliopita baada ya kuishi mafichoni kwa miaka kadhaa.

Kulingana na upande wa mashtaka, wanajeshi wa Ong'wen walihusika katika kuwachinja raia wasio na hatia, kuzichoma nyumba zao na kuiba mali yao.

Image caption Wakazi wa eneo la Lukodi, Gulu wamekusanyika vituo vingi kufuatilia matukio ICC kupitia runinga

Kiongozi wa LRA Joseph Kony ni miongoni mwa wale wanaosakwa sana na mahakama hiyo.

Kundi hilo linatuhumiwa kuwaua zaidi ya watu 100,000 na kuwateka nyara watoto 60,000 katika mgogoro uliochukua takriban miongo mitatu.

Je Ongwen ni nani?

  • Alizaliwa mwaka 1975 eneo la Coorom, kaunti ya Kilak katika wilaya ya Amuru kaskazini mwa Uganda.
  • Inaarifiwa alitekwa nyara na waasi wa LRA akiwa na umri wa miaka 10 wakati alipokuwa anaelekea shuleni Kaskazini mwa Uganda.
  • Miaka iliyofuata, alipanda ngazi na kuwa kamanda
  • Anatuhumiwa kutenda uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo, kuwatumia watoto kama watumwa.
  • ICC ilitoa kibali cha kumkamata mnamo mwaka 2005.
  • Kulikuwa na madai kwamba aliuawa katika mwaka 2013 ambapo Marekani ilitangaza ahadi ya zawadi kwa yeyote mwenye taarifa kumhusu.
  • Alikabidhiwa kwa maafisa wa ICC 16 Januari 2015 na akahamishiwa kizuizi cha ICC tarehe 21 Januari.
  • Alifikishwa kortini mara ya kwanza 26 Januari 2015.