Al-Shabab: Mwandishi aliyekamatwa Kenya huru

Juma
Image caption Juma ameachiliwa huru bila kufunguliwa mashtaka

Mwandishi mashuhuri wa habari za upekuzi nchini Kenya, aliyekamatwa juzi na kuzuiliwa na maafisa wa polisi, ameachiliwa huru bila kufunguliwa mashtaka.

Yassin Juma alikuwa amekamatwa na polisi kuhusiana na kuchapishwa kwa picha za shambulio la wapiganaji wa al-Shabab kambi ya majeshi ya Kenya eneo la el-Ade nchini Somalia.

Wakati wa kukamatwa kwake, polisi waliandika kwamba alikamatwa kwa sababu ya "kutumia vibaya kifaa cha mawasilianoā€¯.

Alizuiliwa usiku kabla ya kufikishwa katika mahakama mjini Kiambu, viungani mwa jiji la Nairobi.

Hata hivyo hakufunguliwa mashtaka na badala yake alirejeshwa katika makao makuu ya idara ya uchunguzi wa jinai na kisha akaachiliwa huru.

Al-Shabab walisema kuwa waliwaua zaidi ya wanajeshi 100 wa Kenya wakati wa shambulio hilo la tarehe 15 Januari, lakini hilo halijathibitishwa.

Image caption Juma ni mmoja wa wanahabari walioripoti kuhusu operesheni ya majeshi ya Kenya nchini Somalia

Serikali bado haijatoa idadi rasmi ya wanajeshi waliouawa au kujeruhiwa.

Habari za kukamatwa kwa Bw Juma zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuibua hamaki miongoni mwa Wakenya, wengi wakitaka aachiliwe huru.

Kitambulisha mada #FreeYassinJuma (Mwachilie huru Yassin Juma) kilivuma sana katika Twitter siku ya Jumapili.