Brazil kutumia jeshi kukabiliana na Zika

Zika Haki miliki ya picha AP
Image caption Watoto karibu 4,000 wamezaliwa wakiwa na vichwa vidogo Brazil

Brazil itatumia wanajeshi zaidi ya 200,000 kukabiliana na mbu wanaoeneza virusi vya Zika ambavyo vimesababisha watoto wengi kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo.

Wanajeshi hao watafika nyumba hadi nyumba wakisambaza karatasi zenye jumbe za kuwahamasisha na kuwashauri wakazi kuhusu virusi hivyo.

Virusi hivyo huenezwa na mbu aina ya Aedes Aegypti.

Waziri wa afya nchini humo Marcelo Castro, amenukuliwa akisema hayo na gazeti la O Globo, ambayo ni ishara ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na taifa hilo dhidi ya virusi vya Zika.

Castro amesema kwamba serikali, ambayo imo katika shinikizo kali kukabiliana na changamoto hiyo, pia itasambaza dawa na mafuta ya kujipaka kuzuia mbu kwa zaidi ya kina mama 400,000 waja wazito.

Image caption Virusi vya Zika huenezwa na mbu aina ya Aedes Aegypti

Virusi vya Zika vinadaiwa kusababisha ugonjwa wa microcephaly, ambapo watoto wanazaliwa wakiwa na vichwa vidogo.

Ongezeko la visa hivyo Amerika Kusini, hasa Brazil, limefanya baadhi ya mataifa, ikiwemo Marekani kuwashauri wanawake waja wazito kutozuru eneo hilo.

Hii ni changamoto kubwa hasa kwa Brazil inapojiandaa kuandaa mashindano ya Olympiki katika mji wa Rio de Janeiro, mwezi Agosti mwaka huu.

Kinyume na maradhi mengine ambayo husababisha wasiwasi mkubwa kimataifa, virusi vya Zika havisambai kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Aidha, kwa watu wengi walioambukizwa, dalili za homa humalizika baada ya kipindi cha wiki moja hivi.

Na kwa watu wengi ambao huambukizwa, ugonjwa huo ambao dalili yake inafanana na homa kali au mafua, humalizika chini ya wiki moja.