Jaji adaiwa kupokea rushwa ya $2m Kenya

Mutunga
Image caption Dkt Mutunga ameitisha kikao cha tume ya mahakama Jumatano

Jaji mmoja wa mahakama ya juu nchini Kenya anachunguzwa kwa madai ya kupokea rushwa ya jumla ya $2 milioni kutoka kwa mwanasiasa.

Jaji huyo anadaiwa kupokea pesa hizo ili kumpendelea mwanasiasa huyo kwenye kesi ya kupinga kuchaguliwa kwake kwenye uchaguzi mkuu wa 2013.

Kiongozi wa idara ya mahakama nchini Kenya, Jaji Mkuu Willy Mutunga amekiri kupokea nyaraka kuhusu malalamiko dhidi ya jaji huyo Novemba mwaka jana.

Amesema uchunguzi wa kina umefanywa na ripoti ya uchunguzi itakabidhiwa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), Tume ya Kupambana na Rushwa na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.

Dkt Mutunga, ambaye majuzi alinukuliwa na gazeti moja la Uholanzi akisema Kenya imeshikwa mateka na “magenge ya wanyang’anyi” na kwamba ufisadi umekita mizizi, ameitisha kikao cha dharura cha JSC.

“Kwa mtazamo wa idara ya mahakama, ukizingatia cheo cha jaji huyu, na uzito wa madai dhidi yake, pamoja na vile kisa hiki kimevutia umma, nitawasilisha suala hili kwa kikao maalum cha JSC Jumatano,” amesema Dkt Mutunga, kupitia taarifa.

Image caption Magazeti mengi Kenya yanaongoza na habari hizo

“Tume ya JSC itaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria na kufuata utaratibu unaofaa," amesema Dkt Mutunga.