Wanajeshi wa Kenya waondoka el-Adde

Somalia Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanajeshi wa Kenya wamekuwa nchini Somalia tangu 2011

Wakazi kusini mwa Somalia wanasema majeshi ya Kenya yameanza kuondoka kutoka eneo la el-Adde ambako kambi ya majeshi hayo ilishambuliwa wiki moja iliyopita. Majeshi hayo pia yameuhama mji wa Badhaadhe.

Ripoti zinasema wanajeshi hao wameondoka el-Adde pamoja na miji mingine ya karibu.

Msemaji wa majeshi ya Kenya Kanali David Obonyo hata hivyo amesema kuondoka kwa wanajeshi hao ni jambo la kawaida.

Wanajeshi karibu 4,000 wamekuwa wakihudumu chini ya majeshi ya Muungano wa Afrika (Amisom) kuisaidia serikali ya nchi hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na tishio kutoka kwa wapiganaji wa Kiislamu wa al-Shabaab.

Wakazi wamekuwa wakilalamikia kunyanyaswa na wanajeshi wa Kenya tangu kushambuliwa kwa kambi hiyo tarehe 15 Januari, na wamefurahia kuondoka kwa wanajeshi hao.

Mbunge mmoja kutoka Somalia ameambia BBC kwamba wanajeshi wa Kenya pia wameondoka kutoka mji wa Badhaadhe.

Ripoti zinasema wanajeshi wa Kenya waliondoka kwenye kambi yao leo asubuhi na kwamba wapiganaji wa al-Shabaab wameonekana mjini humo.

Kanali Obonyo amesema kuondoka kwa wanajeshi hao ni moja moja tu ya mipango ya kijeshi na hakufai kutazamwa kama kuondoka kabisa kwa wanajeshi eneo hilo.

Al-Shabab wanasema waliwaua wanajeshi zaidi ya 100 baada ya kushambulia el-Adde.

Serikali ya Kenya imepuuzilia mbali habari hizo ingawa bado haijatoa takwimu rasmi ya wanajeshi waliouawa au kujeruhiwa.