Uganda yawaokoa wanawake 7 Saudi Arabia

Image caption Uganda yawaokoa wanawake 7 Saudi Arabia

Wanawake 7 raia wa Uganda wamerejeshwa nyumbani baada ya kupatika wakiwa katika hali mbaya nchini Saudi Arabia.

Wengi wao wanadai kudhulumiwa na waajiri wao, kunyimwa mishahara, uhuru na hata haki za kimsingi.

7 hao walikuwa miongoni mwa waganda 24 waliofungwa katika bweni moja la wahamiaji ambalo huwa ni makao ya wageni waliokimbia waajiri wao ama walikuwa nchini Saudia kinyume cha sheria.

Serikali ya Uganda imewarejesha nyumbani wanawake saba raia wa nchi hiyo ambao walikuwa wamekwama nchini Saudi Arabia walikokuwa wamekwenda kutafuta ajira.

Ripoti zinasema kuwa wanawake hao walipatikana katika makao moja ya wahamiaji katika mji mkuu wa Saudia,Riyadh.

Hatua hiyo iliyotangazwa na balozi wa Uganda mjini Riyadh inafwatia kauli ya kufutiliwa mbali uajiri wa vijakazi wa nyumbani kwenda Mashariki ya kati kufuatia madai kuwa wanateswa na waajiri wao mbali na kunyimwa haki zao za kimsingi.

Balozi Sheikh Rashid Yahya Ssemuddu, amesema kuwa wengi wa wasichana hao walipelekwa nchini humo baada ya kuhadaiwa kuwa watapata kazi nzuri.

Wanawake wa Afrika wamekuwa wakienda Saudi Arabia kutafuta ajira baada ya kushinda kupata kazi katika mataifa yao.

Huko Riyadh vijakazi hao hupokonywa vyeti vya usafiri mbali na kunyimwa uhuru wao na hata mishahara yao.

Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Hii sio mara ya kwanza kwa wanawake waAfrika kudai wamedhulumiwa Saudia.

Hii sio mara ya kwanza kwa wanawake waAfrika kudai wamedhulumiwa Saudia, Mwaka uliopita Kenya ilipiga marufuku raia wake kutafuta ajiri nchini humo.

Tanzania nayo imetoa masharti ya kulinda haki za raia wake wanaotafuta ajira nje.

Indonesia, Ethiopia na Philippines pia zimepiga marufu raia wao kwenye nchini Saudi, hadi pale watakapohakikishiwa kuwa haki za kimsingi za kazi zitaheshimiwa.

Balozi huyo alisema juhudi zimewekwa kuzuia wasichana waganda kutosajiliwa na kupelekwa Saudia ambako wanadai hutumika kama watumwa.