Nigeria: Milipuko yaua watu Chibok

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Baadhi ya watu waliojeruhiwa wakipokea matubabu kufuatia shambulio la bomu la siku za nyuma nchini Nigeria

Watu 13 wameuawa nchini Nigeria baada ya wapiganaji watatu wa kujitolea muhanga kujilipua katika mji wa kaskazini mashariki wa Chibok ambapo kundi la Boko Haram liliwateka nyara zaidi ya wasichana 200 wa shule, kulingana na mzee mmoja aliyezungumza na chombo cha habari cha AFP.

Zaidi ya watu 30 wamedaiwa kujeruhiwa baada ya shambulio hilo kulingana na Ayuba Chibok akiongezea kuwa milipuko hiyo ilitokea katika soko.

Mabomu hayo yanadaiwa kulenga maeneo matatu tofauti.

Bomu la kwanza lililipuka katika soko la kila wiki huku jingine likilipuka katika kituo cha barabarani.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mlipuko nchini Nigeria

Haijajulikana bomu la tatu lililipuka wapi.

Mkaazi mmoja wa Chibok ameiambia BBC kwamba walipuaji watano wa kujitolea muhanga waliingia katika mji huo mapema siku ya jumatano huku watatu kati yao wakijilipua.

Wawili waliosalia bado wako katika mji huo kulingana na Malam Ayouba.

''Watu niliozungumza nao bado wameshangaa'', wengine wao bado wanalia,aliambia idhaa ya BBC Hausa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wasichana wa Chibok

Wapiganani kundi la Boko Haram walivamia mji huo mnamo mwezi Aprili 2015 na kuwateka nyara zaidi ya wasichana 200.

Utekaji huo ulizua hisia kali kimataifa.