Makaburi ya pamoja 'yagunduliwa' Burundi

Kaburi Haki miliki ya picha
Image caption Picha moja ya satelaiti ambayo shirika la Amnesty linasema inaonyesha kuwepo kwa kaburi la pamoja

Shirika la Amnesty International limesema limepata picha za satelaiti zinazoonyesha uwepo wa makaburi matano ya pamoja katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura.

Maafisa wa usalama wanadaiwa kuua watu wengi baada ya kuenea kwa machafuko mwezi Desemba.

Amnesty limesema picha hizo zinaonyesha makaburi hayo yaliyozikwa watu wengi kwa pamoja eneo la Buringa viungani mwa Bujumbura.

Shirika hilo limesema uchunguzi wao wa kitaalamu unafanana na ule ambao wameupata kutoka kwa mashahidi kuwa kuna makaburi mengine ya pamoja ya watu waliouwawa siku ya tarehe 11 Desemba, siku ambayo ilishuhudia machafuko makubwa mjini Bujumbura.

Watu zaidi ya 87 waliuawa wakati wa msako uliofanywa na maafisa wa usalama Desemba, baada ya kambi za jeshi kuvamiwa na watu wenye silaha.

Umoja wa Mataifa umesema idadi halisi huenda ikawa juu.

Umoja huo umesema pia unatathmini picha za satelaiti kuchunguza ripoti za kuwepo kwa mataburi tisa ya pamoja, moja katika kambi ya jeshi ambalo linakadiriwa kuwa na miili zaidi ya 100.

Ripoti hiyo ya Amnesty International imetolewa siku chache kabla ya kufanyika mkutano wa viongozi wa umoja wa Afrika kukutana kujadili hatima ya mgogoro wa Burundi huko Ethiopia.

Image caption Bw Nkurunziza amekataa majeshi ya AU yatumwe Burundi

Mgogoro wa Burundi ulianza April mwaka uliopita, wakati Rais Pierre Nkurunzinza alipotangaza kuwa angewania nafasi ya urais kwa awamu ya tatu.

Aliwania ana akachaguliwa tena kuwa rais mwezi Julai.

Watu zaidi ya 439 wameuawa na wengine 240,000 kukimbilia matafa jirani, Umoja wa Mataifa unasema.

Muungano wa Afrika unamtaka Bw Nkurunziza akubali kuwapokea walinda amani wa muungano huo kusaidia nchi hiyo isitumbukie kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Lakini wadadisi wanasema itakuwa vigumu sana kwake kukubali hilo.