Jopo la UN lapendekeza Kiir awekewe vikwazo

Sudan Haki miliki ya picha AFP
Image caption Utekelezaji wa mkataba wa amani Sudan Kusini umekwama

Jopo maalum la Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan Kusini limewasilisha pendekezo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitaka viongozi wa juu nchini humo wawekewe vikwazo.

Miongoni mwao ni Rais Salva Kiir na Kiongozi wa waasi Riek Machar ambao wamedaiwa kuchangia pakubwa katika vita vinavyoendelea Sudan Kusini.

Mshirikishi wa jopo hilo Payton Knopf ameambia BBC kwamba uhalifu unaotekelezwa nchini humo, ikiwemo kuwalenga raia umeamrishwa na Rais Kiir pamoja na Dkt Machar.

Maelfu ya watu wameuawa tangu mapigano kuzuka Sudan Kusini Desemba mwaka 2013 kati ya wafuasi wa viongozi hao wawili.

Aidha karibu watu 2 milioni wamekimbia makwao. Pendekezo hilo limetaka maafisa wengine wa juu wawili kuwekewa vikwazo pia.