WHO yaeleza wasiwasi kuhusu Zika

Chan
Image caption Dkt Chan amesema kuna maswali mengi sana ambayo yanahitaji majibu

Shirika la Afya Duniani limeunda kundi maalum la dharura la kuangazia virusi vya Zika, na kueleza wasiwasi kuhusu kuenea kwa virusi hivyo.

Shirika hilo limesema linatarajia visa vya maambukizi ya virusi hivyo kuongezeka na kufikia milioni tatu au nne katika mataifa ya Amerika.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt Margaret Chan amesema virusi vya Zika “vimepanda kutoka tishio ndogo na kuwa tishio kubwa” na kwamba mlipuko wa virusi hivyo unasababisha madhara makubwa.

Kundi hilo maalum litakutana Jumatatu kuamua iwapo mlipuko wa virusi vya Zika unafaa kutangazwa kuwa dharura ya kiwango cha kimataifa.

Mara ya mwisho dharura ya kimataifa kutangazwa ilikuwa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola Afrika Magharibi ambao uliua watu 11,000.

Virusi vya Zika viligunduliwa mara ya kwanza nchini Uganda mwaka 1947 lakini havijawahi kusababisha mlipuko wa kiasi kikubwa kama sasa.

Huwezi kusikiliza tena

Kisa cha kwanza cha virusi vya Zika nchini Brazil kililipotiwa mwezi Mei 2015.

Wengi wa walioambukizwa hawaonyeshi dalili za kuambukizwa na ni vigumu sana kupima na kubaini iwapo mtu ameambukizwa virusi hivyo.

Hata hivyo, maafisa wa WHO wanakadiria kwamba watu 1.5 milioni wameambukizwa nchini Brazil.

Virusi hivyo, ambavyo huenezwa na mbu, vimesambaa hadi mataifa 20 kanda hiyo.

Aidha, kumetokea ongezeko kubwa la visa vya watoto kuzaliwa na vichwa vidogo, ugonjwa ambao unajulikana kwa Kiingereza kama microcephaly, pamoja na ugonjwa nadra sana wa mfumo wa neva kwa jina Guillain-Barre Syndrome.

Uhusiano kati ya virusi hivyo na maradhi hayo bado haujathibitishwa, lakini Dkt Chan amesema dalili zinaonyesha virusi hivyo ndivyo vinayosababisha matatizo hayo ya kiafya.

Ameonya kuwa hali huenda ikawa mbaya zaidi kwamba hali ya anga ya El Nino ambayo inatarajiwa kukumba maeneo mengi, inatarajiwa kuongeza idadi ya mbu.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Virusi vya Zika vinaaminika kusababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo

Mwandishi wa BBC David Shukman, aliyeko mjini Recife, kaskazini mashariki mwa Brazil anasema madaktari wanazidiwa na visa microcephaly.

Hospitali moja mjini humo imeshuhudia ongezeko la visa kutoka kwa visa vitano kwa mwaka hadi visa 300 katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Awali, madaktari wakiandika katika jarida la kimatibabu la Journal of the American Medical Association wamezema virusi vya Zika vina uwezekano mkubwa wa kusababisha mlipuko mkubwa wa maradhi.

Madaktari hao wamesema hatua ya WHO kukosa kuchukua hatua upesi huenda kulisababisha maelfu ya vifo kutokana na Ebola.