Ufaransa yaitaka Burundi iwaachilie wanahabari

Burundi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Visa vya watu kukamatwa na wengine kuuawa vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara Burundi

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius ameitaka Burundi kuwaachilia huru mara moja wanahabari wawili wa kigeni waliokamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa polisi.

Mmoja wa wanahabari hao ni raia wa Ufaransa.

Mpiga picha Mwingereza Phil Moore na mwanahabari Mfaransa Jean Philippe Remy walikamatwa pamoja na watu wengine 15 Alhamisi jioni katika mtaa wa Nyakabiga ambao ni ngome ya upinzani mjini Bujumbura.

Wawili hao wameshinda tuzo kadha za uanahabari na walikuwa wamesafiri Burundi mara kadha tangu kuanza kwa mzozo wa sasa wa kisiasa nchini humo, mwandishi wa BBC Maud Jullien anasema.

Chama cha wanahabari kutoka nje ya Afrika Mashariki kinasema kinasikitishwa sana na kukamatwa kwa wawili hao ambao kimesema ni "weledi katika kazi ya uanahabari”.

Bw Remy hufanyia kazi gazeti la Le Monde la Ufaransa

Naibu msemaji wa polisi Moise Nkurunziza alikuwa awali amesema wawili hao walikamatwa wakiwa “miongoni mwa kundi la wahalifu”.

Alisema kupitia taarifa fupi kwa wanahabari kwamba “wahalifu” wengine 15, akiwemo mwanamke, walikamatwa na bunduki nne kupatikana.

Polisi bado hawajasema watashtakiwa kwa makosa gani au kama watafurushwa kutoka nchi hiyo.