Mfungwa mtoro arudishwa Marekani

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ethan Couch

Mfungwa mtoro ambaye habari zake ziligonga vichwa vya habari kwa kujitetea kuwa ameathiriwa na "ugonjwa wa matajiri" baada ya kusababisha ajali mbaya pale alipokuwa akiendesha gari akiwa mlevi, amerejeshwa Marekani kutoka Mexico.

Ethan Couch, mwenye umri wa miaka 18, alikuwa amezuiliwa katika gereza la watoto baada ya kuwagonga na kuwauwa watu wanne mwaka 2013.

Mwezi uliopita, yeye na mamaake walitoroka kutoka Texas baada ya kuhepa kifungo hicho. Walikamatwa katika mji wa watalii wa Vallarta nchini Mexico.

Mamake, Tonya Couch,amerejeshwa tayari nchini

Ethan Couch alikata rufaa dhidi ya hatua hiyo ya kurejeshwa kwa nguvu hadi Marekani, lakini siku ya Jumanne aliondoa rufaa hiyo.

Aliwasili Texas Alhamisi asubuhi.

Mwaka 2013 kesi hiyo ya Couch ilikuwa maarufu baada ya mwanasaikolojia mmoja katika kesi hiyo kuohoji kuwa malezi yake ya ufahari yaliwafanya wazazi wake kutomfunza kuwa na hisia ya uajibikaji,hali ya afya inayojulikana kama "ugonjwa wa matajiri".

Couch alihukumiwa miaka kumi katika kituo cha kubadilisha tabia.

Mamake Tonya Couch, anakabiliwa na makosa ya kuzuia kukamatwa kwa mwanawe.