Sanamu ya Cecil Rhodes kusalia chuoni Oxford

Cecil Haki miliki ya picha Flickr
Image caption Cecil Rhodes alikuwa mwanafunzi Oxford

Chuo kimoja kishirikishi cha Chuo Kikuu cha Oxford kimesema hakitaondoa sanamu ya Mwingereza Cecil Rhodes.

Wanaharakati waitaka sanamu hiyo iondolewe, wakisema Rhodes ambaye alikuwa mfanyabiashara na mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa kusini mwa Afrika karne ya 19 alitetea ubabe wa watu weusi.

Rhodes alihusika sana katika kudhibiti maeneo ya Afrika Kusini na Zimbabwe na Zambia zamani zilijulikana na majina yake, zikiitwa Rhodesia Kusini na Rhodesia Kaskazini.

Chuo cha Oriel, kilichoko Oxford nchini Uingereza, kilianzisha mashauriano mwezi uliopita na maafisa wake wanasema wengi wa walioshiriki walikubali sanamu hiyo isalie chuoni.

Maafisa wa chuo hicho wamesema sanamu hiyo ni kumbukumbu ya historia na sifa za ukoloni.

Uamuzi wa chuo hicho umejiri baada ya chama cha midahalo cha Muungano wa Oxford kupiga kura 245 dhidi ya 212 kwa sanamu hiyo kuondolewa mapema mwezi huu.

Kampeni ya ‘Rhodes Must Fall’ (Rhodes lazima aanguke) ilianza Afrika Kusini na mwishowe sanamu ya Rhodes ikaondolewa.

Kampeni hiyo baadaye ilisambaa hadi Oxford.

Haki miliki ya picha GETTY IMAGES
Image caption Sanamu ya Rhodes chuo kikuu cha Cape Town Afrika Kusini iliondolewa

Gazeti la Daily Telegraph limeripoti kuwa uamuzi wa chuo cha Oriel kuhifadhi sanamu hiyo ulifanywa baada ya wafadhili kutishia kuondoa ufadhili wa £100m.

Rhodes alikuwa mwanafunzi Oxford na mwanachama wa chuo cha Oriel miaka ya 1870. Aliachia chuo hicho pesa baada ya kufariki kwake 1902.

Ufadhili wa masomo wenye jina lake kufikia sasa umewafaidi wanafunzi zaidi ya 8,000 ng’ambo.