Kundi laomba wenye Zika waruhusiwe kutoa mimba

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Virusi vya Zika vinaaminika kuchangia kuzaliwa kwa watoto wakiwa na ubongo uliodumaa

Kundi la mawakili, wanaharakati na wanasayansi nchini Brazil limewasilisha ombi mahakama ya juu nchini humo likitaka wanawake wenye virusi vya Zika waruhusiwe kutoa mimba.

Virusi vya Zika vinaaminika kusababisha watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo, na kudumaza ubongo.

Utoaji mimba nchini Brazil hauruhusiwi kisheria, ila tu wakati wa dharura ya kiafya au iwapo mimba imetokana na ubakaji hali ambayo kwa Kiingereza inajulikana kama microcephaly.

Hata hivyo mwaka 2012, uliruhusiwa kwa watu walioathiriwa na ugonjwa mwingine wa ubongo kwa jina anencephaly.

Wataalamu wameonya kwamba idadi ya watu walioambukizwa na virusi vya Zika mwaka huu huenda ikafikia kati ya milioni tatu au nne mwaka huu mabara ya Amerika.

Ombi hilo mpya litawasilishwa mahakama ya juu katika kipindi cha miezi miwili.

BBC imefahamu kwamba kundi hilo linasema serikali ya Brazil imechangia kuenea kwa mlipuko wa sasa wa Zika kwa kutoangamiza mbu aina ya Aedes aegypti ambao wanabeba virusi hivyo.

Wanawake wa Brazil “hawafai kuadhibiwa kutokana na matokeo ya sera dhaifu za serikali”, kundi hilo linasema.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanawake kwa sasa hawaruhusiwi kutoa mimba Brazil

Kundi linaloandaa ombi hilo ndilo lililowasilisha ombi kwa niaba ya waathiriwa wa anencephaly mwaka 2012 mahakama ya juu na kupata ushindi.

Hayo yakijiri, Thomas Bach, mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki amesema hatua zinachukuliwa kulinda michezo ya mwaka huu ambayo itaandaliwa mjini Rio de Janeiro.

IOC itatoa mwongozo baadaye Ijumaa kwa wanariadha na wageni ambao wanapanga kushiriki au kuhudhuria michezo hiyo.

Brazil ndilo taifa lililoathirika zaidi na mlipuko wa Zika.

Kuna visa 270 vya watoto kuzaliwa na vichwa vidogo ambavyo vimethibitishwa, kwa mujibu wa wizara ya afya nchini humo.

Kuna visa vingine 3,448 vya microcephaly ambavyo vinachunguzwa.

Watu wengi huwa hawaonyeshi dalili za kuambukizwa virusi vya Zika lakini wanaweza kusambaza virusi hivyo kwa watoto wao.

Bado hakuna tiba wala chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Marekani imesema inatumai itaanza kufanyia majaribio chanjo kwenye binadamu kufikia mwisho wa 2016.