Kesi ya Gbagbo 'marufuku Equatorial Guinea'

Obiang Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Obiang ameongoza Equatorial Guinea tangu 1979

Runinga ya taifa nchini Equatorial Guinea imezuiwa kupeperusha matangazo kuhusu kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu inayoendelea dhidi ya aliyekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC).

Shirika la habari la ICC limemnukuu afisa wa serikali akisema marufuku hiyo imetolewa kutokana na “urafiki” kati ya Bw Gbagbo na Rais wa Equatorial Guinea Teodoro Obiang Nguema.

Kadhalika, kutokana na sera ya “kutoingilia masuala ya ndani ya taifa jingine”.

Runinga hiyo kwa jina RTNGE, ambayo hupeperusha matangazo kwa lugha ya Kihispania, hutazamwa na asilimia 85 ya raia nchini humo, shirika la AFP linasema.

Wapinzani wa Bw Obiang, ambaye amekuwa uongozini tangu 1979, humtuhumu kuwa mmoja wa viongozi wanaokandamiza upinzani zaidi Afrika.

Bw Gbagbo ndiye kiongozi wa kwanza wa zamani wa taifa kufikishwa ICC.

Anakabiliwa na mshtaka kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2010 nchini Ivory Coast.

Kesi hiyo ilianza Alhamisi wiki iliyopita na imeendelea kusikizwa leo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Gbagbo aliondolewa mamlakani na wapiganaji waliosaidiwa na wanajeshi wa Ufaransa

Mawakili wa Bw Gbagbo, wameiambia mahakama hiyo kwamba kiongozi wa sasa Alassane Ouattara, alichukua madaraka kwa nguvu.

Wanasema Bw Ouattarra, aliyeingia mamlakani baada ya kuondolewa kwa Bw Gbagbo, alisaidiwa na wanajeshi wa Ufaransa.

Watu 3,000 waliuawa kwenye vita kati ya vikosi vya Bw Gbagbo na watu waliomuunga mkono Bw Ouattara.