Magufuli alaani kuuawa kwa rubani porini

Rubani
Image caption Helikopa aliyokuw akiiendesha Gower ilidondoshwa na majangili pori la akiba Maswa

Rais wa Tanzania John Magufuli amesema amesikitishwa sana kitendo cha kuuawa kwa rubani Mwingereza aliyekuwa akisaidiana na maafisa wa Tanzania kupambana na ujangili.

Rubani wa helkopta Kapteni Roger Gower, alifariki baada ya majangili kuifyatulia risasi na kuidondosha helkopta aliyokuwa akiiendesha wakati alipoungana na askari wanyamapori waliokuwa wakikabiliana na majangili katika pori la akiba lililopo katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.

Askari mmoja wa Tanzania alijeruhiwa wakati wa kisa hicho.

Tembo watatu pia walipatikana wakiwa wameuawa.

Dkt Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha waliomuua rubani huyo wanakamatwa na wanafikishwa mikononi mwa vyombo vya sheria, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kurugenzi ya mawasiliano ya ikulu.

Polisi tayari wamewakamata washukiwa watatu kuhusiana na mauaji hayo.

Kiongozi huyo amesema serikali yake itahakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya ujangili kwa nguvu zake zote.

Amewataka wananchi na wadau mbalimbali wa hifadhi ya wanyamapori, kutokatishwa tamaa na tukio hilo na wasaidie kuwafichua watu wote wanaojihusisha na ujangili ama biashara ya bidhaa zitokanazo na ujangili.

Hivi karibuni, utawala nchini Tanzania umekuwa ukikosolewa kwa kushindwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na uwindaji haramu wa pembe za ndovu.

Uwindaji haramu umeenea sana katika pori ya Maswa na sio tukio la kwanza ambapo wanaharakati wanaolinda wanyama wa porini wanashambuliwa na wawindaji haramu.