Kampuni ya Google yaizidi Apple kwa thamani

Google Haki miliki ya picha Getty
Image caption Google imenufaika sana kutokana na matangazo kwenye simu

Kampuni ya Alphabet, inayomiliki Google, imeipita Apple na kuwa kampuni yenye thamani kubwa zaidi duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya mapato ya karibuni zaidi ya kampuni hiyo, faida yake ilifikia $4.9bn (£3.4bn) kwa robo ya tatu ya mwaka, ikipanda kutoka $4.7bn mwaka jana.

Tangazo hilo limesababisha bei ya hisa zake kupanda 9%.

Hii ina maana kwamba Alphabet sasa ina thamani ya $568bn, ikilinganishwa na Apple, ambayo thamani yake ni $535bn.

Hii ni mara ya kwanza kwa Alphabet kutenganisha mapato ya biashara ya Google, ambayo hujumuisha kisakuzi na YouTube, kutoka kwa biashara yake ya "Other Bets" ambayo hujumuisha miradi ya uvumbuzi kama vile magari ya kujiendesha na vipute vya kusambaza huduma za mtandao wa intaneti.

Kwa mwaka, Alphabet ilipata $16.3bn lakini takwimu zinaonyesha biashara yake ya "Other Bets" ilipoteza $3.6bn kipindi hicho, huku mapato ya jumla ya biashara ya Google yakipanda hadi $23.4bn, as kutokana na kuongezeka kwa matangazo mtandaoni.

"Inaonekana Google imeendelea kufanikiwa katika kufaidi kutoka kwa matangazo kwenye simu,” amesema Neil Doshi, meneja mkurugenzi wa utafiti katika kampuni ya Mizuho Securities.

"Miaka miwili au mitatu iliyopita, sekta ya simu ilitatiza sana Google. Kulikuwa na wasiwasi kwamba ingeathiri biashara zilizotegemea kompyuta, lakini huku simu sikianza kutumiwa sana kuchakura mtandaoni, matangazo kwenye simu yanakaribia yale ya kompyuta za kawaida kwa thamani.”