Meli iliyokuwa hatarini yarejeshwa baharini

Meli Haki miliki ya picha Marinha Francesa
Image caption Meli hiyo kwa jina Modern Express imevutwa na kurejeshwa ndani ya bahari

Meli iliyokuwa ikielekea kwenye ufuo wa Ufaransa ikiwa imeinama imerejeshwa ndani ya bahari, maafisa wa baharini wanasema.

Meli ya kuvuta meli nyingine kutoka Uhispania imefanikiwa kuivuta meli hiyo na kuiingiza ndani ya baharini, msemaji wa chama cha mabaharia Ufaransa Louis-Xavier Renaux amesema.

Meli hizo mbili sasa zinaelekea magharibi ndani ya bahari ya Atlantic kwa kasi ya kilomita tano kwa saa, ameongeza.

Mabaharia 22 waliokuwa kwenye meli hiyo kwa jina Modern Express ambayo imesajiliwa Panama, waliondolewa salama kwa kutumia ndege kutoka kwenye meli hiyo Jumanne wiki iliyopita.

Maafisa walikuwa wamehofia kwamba meli hiyo, iliyokuwa kilomita 44 pekee kutoka ufuo wa Ufaransa eneo la Arcachon karibu na Bordeaux, ksuini magharibi mwa Ufaransa ingezama.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mabaharia wote waliokolewa kwa kutumia ndege

Lakini wataalamu wane walifanikiwa kushikisha mnyororo wa kuvuta meli hiyo na kuwezesha kuvutwa kwake.

Iwapo operesheni hiyo ingefeli, meli hiyo ingegonga ufuo wa kusini magharibi mwa Ufaransa kati ya Jumatatu usiku na Jumanne asubuhi.

Hali mbaya ya hewa ilitatiza juhudi za uokoaji Jumapili, siku mbili baada ya mnyororo mwingine wa kuivuta meli hiyo kukatika.

Haki miliki ya picha ReutersMarine Nationale
Image caption Kuchafuka kwa bahari kulitatiza juhudi za kuiokoa meli hiyo

Meli hiyo ilikuwa imebeba tani 3,600 za mbao na mashine za kuchimba ardhini.

Ilikuwa imeinama kwa pembe ya nyuzi 40 hadi 50.

Maafisa wa baharini wamesema haiwezekani kuisimamisha.

Haki miliki ya picha AP

Meli hiyo ina mafuta tani 300 na kwa mujibu wa gazeti la Sud-Ouest, mipango ya dharura ilikuwa imeandaliwa kuhifadhi na kuyatoa mafuta hayo iwapo ingezama.