Ted Cruz: Ushindi wetu Iowa hauna kifani

Trump Haki miliki ya picha Getty
Image caption Trump alikuwa akiongoza kwenye kura za maoni

Seneta wa Texas Ted Cruz ambaye amemshinda Donald Trump kwenye mchujo wa chama cha Republican jimbo la Iowa amesema ushindi huo hauna kifani.

Akizungumza na runinga ya CNN, seneta huyo amesema ushindi huo umempa msukumo kabla ya michujo kata majimbo mengine kufanyika.

“Tuna matumaini tunapoelekea New Hampshire, South Carolina ... ninaangazia ushindi wetu.”

Senator Cruz pia amesifu wafuasi wake mashinani kwa ushindi wake.

Alipoulizwa mpinzani wake mkuu ni nani katika chama cha Republican, amesema anapenda na anawaheshimu wapinzani wote katika kinyang’anyiro hicho.

Huo ulikuwa ndio mchujo wa kwanza katika uchaguzi wa urais wa 2016 ambao utafanyika baadaye mwezi Novemba.

Cruz alipata asilimia 28 ya kura.

"Huu ni ushindi wa wahafidhina jasiri," mgombea huyo alisema.

Mfanyabiashara Donald Trump alikuwa akiongoza kwenye kura za maoni kabla ya kura kupigwa lakini alimaliza wa pili na asilimia 24.

Seneta wa Florida Marco Rubio alifanya vyema kuliko ilivyotarajiwa, na akamaliza nambari tatu na asilimia 23.

Matokeo ya Iowa

Chama cha Republican, 100 % ya kura:

  • Ted Cruz: 26%, wajumbe 8
  • Donald Trump: 23%, wajumbe saba
  • Marco Rubio: 23%, wajumbe saba
  • Ben Carson: 10%, wajumbe watatu
  • Rand Paul, Jeb Bush: mjumbe mmoja kila mmoja.
  • Chris Christie, Carly Fiorina, Jim Gilmore, Mike Huckabee, John Kasich and Rick Santorum: hawajapata wajumbe

Chama cha Democratic, 100% ya kura:

  • Hillary Clinton: 49.8%, wajumbe 22
  • Bernie Sanders 49.6%, wajumbe 21
  • Martin O’Malley 0.5%, wajumbe 0

Mgombea anayepigiwa upatu katika chama cha Democratic Hillary Clinton alikabiliana bega kwa bega na mshoshialisti Bernie Sanders, tofauti kati yao ikiwa 0.2% pekee.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Clinton amefurahia ushindi huo

Akizungumza baada ya kubainika kwamba alikuwa ameshinda, Bi Clinton alisema amefurahishwa sana na ushindi huo na kuwashukuru wafuasi wake.

Akizungumza baada ya matokeo kujulikana, Marco Rubio amempongeza Bw Cruz na kusema ndiye mgombea ambaye anaweza kuunganisha chama cha Republican ambacho kimegawanyika.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Bw Trump amempongeza Bw Cruz

Dakika chache baadaye, Bw Trump alipanda jukwaani katika ukumbi mwingine na kumpongeza seneta huyo wa Texas, na kusema anaridhika kumaliza katika nambari mbili.

Wagombea wawili wamejiondoa kinyang’anyironi.

Duru za karibu na mgombea wa Democratic Martin O'Malley, aliyekuwa gavana Maryland, zimeambia BBC kwamba atasitisha kampeni yake, na kufanya ushindani mkali sasa kuwa kati ya wagombea wawili.

Upande wa Republican, gavana wa zamani wa Arkansas Mike Huckabee aliandika kwenye Twitter kwamba atasitisha kampeni yake.