Zika:Watoto 3,670 wachunguzwa Brazil

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Brazil yachunguza visa vya watoto kuzaliwa na vichwa vidogo

Wizara ya afya nchini Brazil inachunguza matukio 3,670 yanayoshukiwa kuwa ya watoto waliozaliwa na vichwa vidogo wakihusishwa na virusi vya Zika, taarifa hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Serikali.

Mpaka sasa Watoto 404 pekee wamethibitishwa kuwa na vichwa vidogo, hali inayosababisha dosari kwenye ubongo.

Idadi hiyo imeongezeka kutoka juma lililopita ambapo idadi ilikuwa Watoto 270.

Tangazo lilisema kuwa watoto 709 waliokuwa wakifanyiwa uchunguzi walibainika kuwa hawakuwa na dosari kwenye ubongo.

Ripoti hiyo ilifafanua kuwa idadi ya awali ya watoto walio na vichwa vidogo ilikuwa 4,783 lakini kwa kuwa 709 waligundulika kutoathirika na 404 kuthibitishwa kuathirika idadi iliyobaki ya waliokuwa wanachunguzwa ni 3,670.

Pia Wizara ya Afya imethibitisha kuwa kesi ya vifo vya watoto 76 vimetokea kutokana na vichwa vidogo, wakati wa ujauzito yaani mimba kutoka, au mara baada ya kuzaliwa kabla ya wakati.