Katanga kujibu mashtaka upya DRC

Image caption Germain Katanga kujitetea mahakamani DRC

Aliyekuwa kiongozi wa waasi nchini jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliyefungwa na mahakama ya ICC, Germain Katanga anatarajiwa kuwasilisha utetezi wake na orodha ya mashahidi mbele ya mahakama moja ya kijeshi nchini humo.

Bwana Katanga alihukumiwa jela miaka 12 jela na mahakama ya ICC na alikuwa ametarajiwa kuachiliwa huru mwezi uliopita lakini maafisa wa mahakama wa DRC walitangaza kuwa atashtakiwa kwa makosa mengine.

Germain Katanga alikuwa kiongozi wa kundi la waasi katika mkoa wa Ituri Mashariki mwa jamhuri ya Congo, miaka ya elfu mbili, wakati mahakama ya kimataifa ya Jinai ICC, alipopatikana na hatia ya mauaji, mashambulizi dhidi ya raia na uharibifu wa mali.

Lakini alipofikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi, Katanga alionekana mtulivu huku akiwa ameketi kwenye kiti kimoja kilichoundwa kwa chuma.

Wale wanaomfahamu wanasema Katanga, ameghadhabishwa kuwa idara ya haki nchini humo, ilijaribu kuzuia kuachiliwa kwake January tarehe kumi na nane.

Akiwa pamoja wa wanachama wengine sita wa waasi, Katanga alisikiliza mashtaka yote dhidi yake ikiwa ni pamoja na uhalifu wa kivita, ukatili dhidi ya binadam na kushiriki katika vugu vugu la uasi.

Shirika la kutetea haki za kibinadam la Human Rights Watch lenye makao yake nchini Marekani, limesema kuwa, Katanga hakupewa muda wa kutosha kujiandaa kwa kikao cha leo.

Shirika hilo limesema notisi iliyotolewa ilikuwa fupi na mshukiwa huyo hangekuwa na nafasi ya kutosha kujibu mashtaka ya kiwango hicho yanayomkabili.

Aidha limetoa wito kwa serikali ya DR Congo, kuwasilisha habari zote kuhusu kesi hiyo kwa mahakama ya kimataifa ya jinai, ili iamue ikiwa itamfungulia mashtaka mapya bwana Katanga.

Hii ni kesi ya kwanza ambayo mtu aliyefunguliwa mashtaka na mahakama ya kimataifa na kuhukumiwa, anafunguliwa mashtaka zaidi katika taifa lake, na wachanganuzi wanasema kesi hiyo itakuwa kipimo cha jinsi mfumo wa haki na idara ya mahakama nchini DR Congo ulivyo na uwezo wake wa kusikiliza kwa uwazi kesi za washukiwa wanaokabiliwa na uhalifu wa kimataifa.