Uber: Waendesha teksi watishia kugoma Nairobi

Image caption Wamiliki wa magari ya teksi mjini Nairobi wanatishia kugoma ilikuishinikiza serikali kuipiga marufuku huduma ya teksi ya Uber

Wamiliki wa magari ya teksi mjini Nairobi wanatishia kugoma ilikuishinikiza serikali kuipiga marufuku huduma ya teksi ya Uber

Msemaji wao Mwangi Mubia ameiambia Capital FM mjini Nairobi kuwa ''Hawana njia nyengine ya kusuluhisha mgongano kati yao na wenye magari wanaotumia huduma hiyo ya mtandao wa Uber.'

''Hawawezi kututuhumu kwa kuwashambulia ilihali ni wao wanaojaribu kutuondoa katika biashara yetu''

''Ni sisi tunaostahili kulalamika mbinu zao mbaya za kupunguza gharama ya usafiri na kwa kiasi kikubwa kutunyima njia ya kujipatia riziki.'' alifoka Mubia.

Hayo yanajiri wakati ambao serikali sasa inajiandaa kuwafikisha mahakamani madereva wawili wa teksi waliokamatwa kwa madai ya kuwashambulia wapinzani wao wanaotumia huduma ya Uber.

''Kwa hakika hata sisi tunajiandaa kuzindua huduma yetu ya teksi ilikuwafaidisha wateja wetu''.

''Iwapo serikali haitasikia maombi yetu basi hatuna budi ila kuwataka wanachama wetu kuegesha magari yao katika makutano yote ya barabara za mji wa Nairobi karibuni iwapo serikali haitaingilia kati kusitisha huduma hiyo''

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Uber: Waendesha taxi watishia kugoma Nairobi

''Walifukuzwa katika mataifa mengine na mji mingi mikuu, kwanini ?''

''Kwa sababu wanawanyima maelfu ya watu mkate wao wa kila siku'' alisema Mubia

Serikali ya Kenya imeonya kuwa ushindani wa kibiashara haupaswi kutumika kuvunja sheria.

Msemaji wa Uber Samantha Allenberg alisema kuwa wamekuwa wakifanya mazungumzo na shirikisho la wenye teksi kwa nia ya kutatua mzozo huo unaotokota.