Trump ataka mchujo wa Iowa urudiwe

Trump Haki miliki ya picha Getty
Image caption Trump anasema Cruz alitumia ulaghai kushinda Iowa

Donald Trump anataka uchaguzi wa mchujo wa kuteua atakayegombea urais kupitia chama cha Republican katika jimbo la Iowa urudiwe, akisema mshindi Ted Cruz alitumia ulaghai.

Bw Trump anasema wakati wa kikao cha Iowa, maafisa wa kampeni wa Cruz waliwaambia wapiga kura kwamba mgombea mwingine Ben Carson alikuwa amejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho, habari ambazo hazikuwa za kweli.

Maafisa wa kampeni wa Cruz baadaye walimuomba radhi Carson, wakisema lilikuwa kosa lisilokusudiwa.

Bw Trump alimaliza wa pili katika mchujo huo wa kwanza kufanyika nchini humo kwa ajili ya uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Mchujo utakaofuata utafanyika New Hampshire Jumanne ijayo.

"Ted Cruz hakushinda Iowa, aliiba. Hii ndiyo maana kura zote za maoni zilionekana kukosea na ndiyo sababi alipata kura nyingi kuliko ilivyotarajiwa. Ni vibaya!,” Bw Trump amesema.

Awali, alikuwa ameandika kwenye Twitter kwamba Bw Cruz alishinda mchujo wa Iowa kwa njia haramu, lakini baadaye akafuta ujumbe huo.

Matamshi ya Bw Trump ni kinyume na hotuba yake ya kukubali kushindwa ambayo aliitoa Jumatatu usiku baada ya matokeo kujulikana, jambo ambalo lilishangaza wengi ikizingatiwa ukali wake.

Bw Trump baadaye alikuwa ameandika ujumbe kwenye Twitter akionekana kuridhika na nafasi ya pili.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Bw Cruz alishangaza wengi kwa kushinda Iowa

Kambi ya Cruz haijafurahishwa na madai ya sasa ya Bw Trump.

“Ukweli umemfika nyota huyu wa runingani – alishindwa Iowa na sasa hakuna anayezungumza kuhusu ubabe wake, kwa hivyo anachomoza kwenye Twitter,” afisa wa mawasiliano wa Bw Cruz Rick Tyler aliandikia Politico kupitia barua pepe.

“Kuna makundi yanayosaidia watu kudhibiti uraibu wa kutumia Twitter, labda anafaa kuwasiliana na tawi moja.”

Katika historia, haijatokea uchaguzi wa mchujo ukarudiwa.

Bw Carson alikubali ombi la msamaha kutoka kwa Bw Cruz lakini maafisa wake wa kampeni wamesema kambi ya Cruz ilitumia “mbinu chafu”.

Jumatano, seneta wa Kentucky Rand Paul na seneta wa zamani wa Pennsylvania Rick Santorum walijitoa kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta tiketi ya chama cha Republican baada ya kutofanya vyema Iowa.