Jopo la UN 'lakubali ombi la Julian Assange’

Assange Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Assange anahofia huenda akakabidhiwa kwa maafisa wa Marekani

Jopo la Umoja wa Mataifa lililokuwa likichunguza kuzuiliwa kwa mwanzilishi wa Wikileaks Julian Assange limekubali malalamiko yake, BBC imefahamu.

Assange alikimbilia ubalozi wa Ecuador mjini London mwaka 2012 kuzuia asikabidhiwe kwa maafisa wa Sweden akajibu mashtaka ya unyanyasaji wa kingono.

Mwaka 2014, alilalamika kwa jopo hilo akisema anazuiliwa kinyume cha sheria kwa sababu hawezi kuondoka ubalozini bila kukamatwa.

Jopo hilo la UN litatoa rasmi ripoti yake kesho Ijumaa.

Kibali cha kumkamata kimekuwepo na polisi nchini Uingereza wamekuwa wakisisitiza kwamba atakamatwa iwapo ataondoka ubalozi huo.

Awali, alikuwa amesema kwamba atajisalimisha kwa polisi Ijumaa iwapo jopo hilo la UN lingeamua kwamba amezuiliwa kwa njia halali.

Shirika la Wikileaks lilichapicha stakabadhi za siri zaserikali ya Marekani mtandaoni na Bw Assange anasema anaamini Washington itajaribu kumkamata na kumfungulia mashtaka iwapo atakabidhiwa kwa maafisa wa Sweden.