Afrika Mashariki yakataa kuitenga Burundi

Image caption Viongozi wa Afrika mashariki

Bunge la Afrika Mashariki halitaitenga Burundi katika jamii ya Afrika Mashariki.

Hatua hiyo inajiri baada ya mswada kuwasilishwa na Muungano wa mawakili wa Afrika pamoja na wanaharakati wa Afrika wakisema kwamba Burundi inafaa kutopewa uongozi wa Jamii ya Afrika mashariki hadi pale taifa hilo litakapomaliza mgogoro uliosababishwa na rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu.

Na baada ya saa sita za kujadiliana ,kamati ya maswala ya kieneo na utatuzi wa migogoro ilitoa ripoti yao kuhusu kuzorota kwa haki za kibinaadamu nchini humo.

Ombi hilo kutoka kwa muungano huo wa mawakili ,linapendekeza hatua kadhaa ikiwemo kuondolewa kwa Burundi kutoka kwa jamii ya Afrika mashariki na badala yake kuliwekea vikwazo taifa hilo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Machafuko Burundi

Abdullahi Mwinyi,ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya maswala ya kieneo na utatuzi wa migogoro amesema kuwa kuiondoa Burundi sio mahitaji ya eneo hili.

Wiki iliopita Muungano wa Afrika ulifutilia mbali pendekezo la kupeleka wanajeshi 5000 wa Umoja wa Afrika ili kukabiliana na mgogoro unaoendelea.

Badala yake AU ilipendekeza ujumbe wa hadhi ya juu kupelekwa mjini Bujumbura ili kijadili suluhu itakayokubalika na rais Nkurunziza.