Somalia: Wanajeshi wa AU waondoka Merca

Image caption Wanajeshi wa Umoja wa Afrika

Ripoti za raia wa Somalia zinasema kwamba wanajeshi wa Umoja wa Afrika wanaoshirikisha wanajeshi wa Uganda wameondoka katika kambi moja katika mji wa bandari ya zamani wa Merca, katika kusini mwa mkoa wa Shebelle ya chini.

Kambi hiyo ipo kilomita 109 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Mogadishu.

Kikosi hicho cha Umoja wa Afrika hata hivyo kimekanusha habari hizo kupitia ukurasa wake kwenye Twitter na kusema ni "propaganda" inayoenezwa na maadui.

"Wanajeshi wetu mara kwa mara watabadilisha mpangilio wake, hii ikiwa ni mbinu ya kuwashinda magaidi," umoja huo umesema.

Ripoti nyengine zinasema kuwa wapiganaji wa al-Shabab walionekana wakiinua bendera yao katika mji huo.

Hatua hii inajiri wakati ambapo wanajeshi wa Kenya wamejiondoa katika kambi kadhaa katika eneo jingine la kusini mwa taifa hilo kufuatia shambulio katika kambi ya el-Ade mwezi uliopita.