Jaji wa mahakama ya juu Kenya apatikana na hatia

Jaji
Image caption Jaji Tunoi amekanusha madai yaliyotolewa dhidi yake

Jaji mmoja wa Mahakama ya Juu nchini Kenya Phillip Tunoi amepatikana na hatia ya kukiuka maadili ya kazi baada ya uchunguzi uliofanywa na kamati iliyoundwa na Tume ya Huduma za Mahakama.

Jaji Tunoi amepatikana na hatia ya "kujihusisha kwa njia isiyofaa" na mtu ambaye alikuwa akimwakilisha mhusika katika kesi ya uchaguzi, jambo amablo ni ukiukaji wa maadili.

Jaji Mkuu Willy Mutunga amempendekezea Rais Uhuru Kenyatta aunde jopo maalum kwa mujibu wa Katiba.

Jopo hilo litakuwa na jukumu la kuchunguza kikamilifu madai yaliyotolewa dhidi ya Jaji Tonui.

Kwa mujibu wa katiba, Jaji wa Mahakama ya Juu anaweza tu kuondolewa kazini baada ya kuchunguzwa na jopo.

Ripoti ya kamati hiyo iliyofanya uchunguzi kwa kipindi cha wiki moja inasema madai ya ulaji rushwa dhidi ya jaji huyo hayajaweza kuthibitishwa, na hilo sasa limeachiwa jopo kuchunguza.

Jaji huyo anatuhumiwa kupokea hongo ya $2 milioni ili apendelee upande mmoja kwenye kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero.

Dkt Kidero na Jaji Tunoi wote wawili wamekanusha madai hayo.

Iwapo atapatikana na hatia na kuondolewa afisini, atakuwa jaji wa pili wa Mahakama ya Juu kuondoka afisini kwa madai ya kukiuka maadili.

Naibu Jaji Mkuu wa zamani Nancy Baraza alijiuzulu Januari 2012, baada ya jopo kuundwa kuchunguza madai kwamba alimnyanyasa mlinzi wa kike katika jumba moja la biashara jijini Nairobi.