Magari ya Sisi yatandikiwa zulia mjini Cairo

Image caption Magari ya Sisi yatandikiwa zulia mjini Cairo

Je umeweka zulia nyumbani kwako ?

Bila shaka umewaona viongozi na marais wakitembea na viatu kwenye mazulia nyekundu .

Amini usiamini rais wa Misri ametandikiwa zulia ili msafara wake wa magari yasikanyage lami!

Barabara ambayo msafara wa magari ya rais Abdul Fattah al-Sisi alipaswa kutumia ulitandikiwa zulia mjini Cairo katika kitongoji kimoja alichokuwa amekwenda kuhudhuria hafla moja siku ya Jumamosi.

Maelfu ya watumizi wa mitandao ya kijamii wamelalamikia vikali gharama ya juu iliyotumika kununua mazulia hayo yote ilhali serikali imekuwa ikilalamika kuwa imekumbwa na ukosefu wa fedha za kufidia kodi ya mafuta ya taa na umeme.

Jeshi lilijitetea likisema kuwa zulia hiyo nyekundu ilikuwa ya ''kuwaletea furaha na raha wamisri ambao wamekuwa na matatizo chungu nzima''

Wenyeji waliokosoa ubadhirifu huo wa mali ya umma waliuliza itakuwaje kuwa mazulia hayo makubwa yatawaletea furaha wamisri ilhali hawakuruhusiwa kuyakanyaga ?''

Mwandishi na mtangazaji wa runinga ya On Tv Youssef al-Husseini, alikejeli hotuba ya rais Sisi huku maelfu ya wamisri maskini wakikosa hata blanketi ya kujizuia baridi kali.

Image caption Barabara ambayo msafara wa magari ya rais Abdul Fattah al-Sisi alipaswa kutumia ulitandikiwa zulia mjini Cairo

Youssef al-Husseini, mwanachama wa vuguvugu la kisosholisti (Revolutionary Socialist movement) aliandika kwenye mtandao wa Facebook kuwa

''Leo nimemshuhudia al Sisi akikanyagakanyaga mali ya umma''

Wakosoaji wa al Sisi wamekuwa wachache mno tangu ampindue rais Mohammed Morsi mwaka wa 2013, lakini swala hili limewasisimua hata waandishi wakuu wa habari nchini humo.

Brigedia Ihab al-Qahwaji, ambaye ni mkuu wa maadili wa jeshi alisisitiza kuwa zulia hiyo ilikuwa nzee na kuwa haikugharimu pesa zozote.

''Ilikuwa zulia iliyotumika kwa zaidi ya miaka 3 na itaendelea kutumika '' alisema bregedia huyo kwenye runinga ya CBC .

"Bila shaka wanaotukosoa ni wengi ila ni wajibu wetu kutoa taswira nzuri ya Misri''. aliongezea Brigedia Ihab.