Obama kuomba $1.8bn za kukabili Zika

Mbu Haki miliki ya picha Getty
Image caption Virusi vya Zika vinaenezwa sana na mbu

Serikali ya Rais Obama imesema itaomba $1.8bn (£1.25bn) kutoka kwenye bunge za kutumiwa kukabiliana na virusi vya Zika.

Virusi hivyo, ambavyo sana vinaenezwa na mbu, vinasambaa kwa kasi sana Amerika.

Virusi hivyo vimehusishwa na visa vya watoto kuzaliwa wakiwa na hichwa vidogo na ubongo uliodumaa.

Pesa hizo zitatumiwa katika juhudi za kuangamiza mbu pamoja na kufadhili utafiti wa kutafuta chanjo dhidi ya virusi hivyo.

Ikulu ya White House imesema sehemu ya pesa hizo itatumiwa “kuongeza uwezo wa nchi zilizoathiriwa na Zika kukabiliana na mbu na kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.”

Kwa sasa, virusi hivyo vimo katika nchi 26 za bara Amerika.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Virusi hivyo vinaaminika kusababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Marekani (CDC) kimethibitisha kwamba visa 50 vya maambukizi ya virusi hivyo vimethibitishwa katika Wamarekani ambao walikuwa wamesafiri maeneo yaliyo na virusi hivyo.

Kuna wasiwasi kwamba huenda mbu wakaongezeka miezi ijayo yenye joto na kuongeza hatari ya kuenea kwa virusi hivyo.

Wiki iliyopita, kisa cha kwanza cha virusi hivyo kusambazwa Marekani kiliripotiwa Dallas, Texas.

Kisa hicho kilitokea kupitia kushiriki mapenzi, badala ya kuumwa na mbu kama ilivyo katika visa vingi.

Virusi hivyo vimeathiri sana Brazil, ambayo imeshuhudia ongezeko la watoto wanaozaliwa na vichwa vidogo miezi ya karibuni.

Visa hivyo vimefikia 4,000 na kuzua wasiwasi huku taifa hilo likitarajiwa kuandaa Michezo ya Olimpiki mwezi Agosti.