Wachezaji wa DR Congo watuzwa magari ya kifahari

Gari
Image caption Kila mchezaji ametunukiwa gari la $60,000

Wachezaji wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamezawadiwa magari ya kifahari baada ya kushinda Kombe la Taifa Bingwa Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani (CHAN).

Rais Joseph Kabila amemtunuku kila mchezaji gari gari la kifahari aina ya Toyota Prado la thamani ya $60,000 (£40,000).

Wachezaji hao pia wamepewa nishani, kwenye hafla iliyoandaliwa ikuluni.

"Asanteni sana kwa ushindi huu. Mmewaunganisha Wakongomani wote," alisema Rais Kabila.

Chui hao wa Kinshasa walitwaa kombe kwa kulaza Mali 3-0 kwenye fainali na kuwa taifa la kwanza kushinda kombe hilo mara mbili.

Mwaka 2009, mara ya kwanza kuandaliwa kwa michuano hiyo, DR Congo waliondoka na ubingwa kwa kulaza Black Stars ya Ghana 2-0 kwenye fainali.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption DR Congo walilaza Mali 3-0 kwenye fainali

Mwandishi wa BBC Mbelechi Msochi anasema mchezaji Heritier Luvumbu Nzinga aliyeumia kwenye michuano hiyo pia ameahidiwa kwamba atasafirishwa ng'ambo kwa matibabu.

Image caption Rais Kabila amewapongeza wachezaji wa timu ya taifa