Korea Kaskazini yafufua mtambo wa nyuklia

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mtambo wake wa kinyuklia kwa nia ya kuzalisha madini ya Plutonium.

Korea Kaskazini imeuwasha mtambo wake wa kinyuklia kwa nia ya kuzalisha madini ya Plutonium.

Mkuu wa idara ya ujasusi wa Marekani James Clapper amesema kuwa kuwashwa upya kwa mtambo huo utaiwezesha kuzalisha madini hayo ambayo ni pembejeo muhimu katika uzalishaji wa silaha za kinyuklia.

Bwana Clapper anasema kuwa Korea Kaskazini imepiga hatua kubwa katika kuafikia azimio lake la kumiliki silaha za kinyuklia yenye uwezo wa kulipua maeneo katika bara ya pili.

Taarifa hiyo imetolewa siku chache tu baada ya Korea Kaskazini kulipua roketi mwishoni mwa juma kwenda anga ya juu.

Wakosoaji wa Korea Kaskazini wakiwemo Marekani, Korea Kusini na Japan wanasema japo ni ukweli kuwa Korea Kaskazini imefaulu kuwasilisha mtambo wake wa satelaiti katika anga ya mbali, hiyo ni njama yao ya kufanya majaribio ya uwezo wake wa kufyatua makombora yenye uwezo wa kusafiri mbali.

Mwezi Septemba mwaka uliopita, Pyongyang ilitangaza kuwa imefufua mtambo wake wa kinyuklia wa Yongbyon.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mtambo huo ndio unaozalisha makaa ya nyuklia na madini ya plutonium ambayo ndio nguzo muhimu ya kuzalisha silaha za kinyuklia.

Mtambo huo ndio unaozalisha makaa ya nyuklia na madini ya plutonium ambayo ndio nguzo muhimu ya kuzalisha silaha za kinyuklia.

Pyongyang imefanya majaribio manne tangu mwezi Januari.

Bwana Clapper anaonya kuwa Pyongyang imeweka nia ya kuunda silaha za kinyuklia zenye uwezo wa kufika Marekani.

Watafiti wanasema kuwa mtambo huo wa Yongbyon unaweza kuzalisha madini muhimu ya plutonium inayoweza kuunda bomu moja la kinyuklia kwa mwaka.

Takriban kilo 4 za plutonium zinahitajika kuunda bomu moja yenye uwezo wa kilo elfu 20,000.