Obama aidhinisha sheria ya kueneza umeme Afrika

Obama Haki miliki ya picha AFP
Image caption Obama alipigia debe mpango huo alipozuru Afrika mwaka jana

Rais wa Marekani Barack Obama ameidhinisha mpango unaolenga kuwafikishia umeme watu 50 milioni kusini mwa jangwa la Sahara kuwa sheria.

Mpango, ambao sasa umekuwa Sheria ya Kufikisha Umeme Afrika ya 2015, unapanga kufikisha umeme kwa watu hao kufikia 2020.

Ni sehemu ya mpango mkubwa wa Bw Obama wa kutaka kufikisha umeme kwa watu zaidi barani Afrika kupitia ushirikiano katika ya serikali na mashirika ya kibinafsi.

Mpango huo umechukua karibu miaka miwili kupitishwa na mabunge yote mawili ya Bunge la Congress.

Karibu theluthi mbili ya watu Afrika hawana umeme wa kutegemewa.

Wadadisi wanasema sheria hiyo mpya huenda ikawezesha mpango huo kuendelezwa na serikali hata baada ya Bw Obama kuondoka White House mapema mwaka 2017.

Mpango huo una lengo la muda mrefu la kuongeza maradufu idadi ya watu walio na umeme Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Haki miliki ya picha GETTY IMAGES
Image caption Kufanywa sheria kwa mpango huo kutahakikisha unaendelea hata baada ya Obama kuondoka madarakani

Sheria hiyo “itaboresha maisha ya mamilioni ya watu kwa kupunguza utegemeaji wa kawi ya mkaa na kawi nyingine zinazochafua mazingira. Hizi huua watu wengi kushinda Ukimwi na Malaria kwa pamoja,” amesema mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kigeni katika bunge la Marekani Ed Royce.

Kampuni ya ushauri wa usimamizi ya McKinsey inakadiria kwamba itagharimu $835bn (£575bn) kufikisha umeme kwa watu wote Afrika kufikia 2030.

Kando na serikali ya Marekani, serikali za nchi za Afrika, washirika wa kimaendeleo, na wahudumu katika sekta ya kibinafsi wote wanahusishwa katika mpango huo mkubwa uliopewa jina Power Africa.

Serikali ya Marekani imetoa $7bn za kusaidia mradi huo, ambao serikali hiyo inasema umepokeza ufadhili wa kiasi cha ziada cha $43bn kutoka kwa wadau mbalimbali.