Virusi vya Zika vyafika Uchina

Zika Haki miliki ya picha Thinkstock
Image caption Virusi vya Zika vinaenezwa na mbu

Mwanamume wa umri wa miaka 34 amekuwa wa kwanza kupatikana na virusi vya Zika nchini Uchina, shirika la habari la serikali limesema.

Mwanamume huyo alirejea majuzi kutoka safarini Amerika Kusini.

Tume ya Taifa ya Afya na Uzazi wa Mpango imesema mwanamume huyo anatoka eneo la Ganxian, katika mkoa wa masharikiwa Jiangxi, shirika la habari za Xinhua limesema.

Virusi hivyo vimehusishwa na kuzaliwa kwa watoto wenye vichwa vidogo na ubongo uliodumaa.

Maafisa nchini Uchina wamesema hakuna hatari kubwa ya virusi hivyo kuenea huko kwa sababu kwa sasa ni majira ya baridi.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Virusi hivyo vinaaminika kusababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo

Virusi hivyo huenezwa sana na mbu.

Mwanamume huyo alikuwa amezuru Venezuela na alirejea kupitia Hong Kong na Shenzhen.

Kwa sasa amewekwa karantini katika hospitali moja Ganxian ambapo anaendelea kupata nafuu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza dharura ya kimataifa ya afya kuhusiana na ugonjwa huo.

Kwingineko nchini Australia, katika jimbo la Queensland, mwanamke mjamzito amethibitishwa kuwa na virusi hivyo.

Alirejea majuzi kutoka ziara ng’ambo na aligunduliwa kuwa na virusi hivyo Jumanne.

Ndiye mtu wa tatu kupatikana na virusi hivyo nchini Australia.

Watu hao wengine wawili waliambukiwa wakiwa nje ya nchi.