Wanajeshi wa AU wanafanikiwa Somalia?

Somalia Haki miliki ya picha AP
Image caption Idadi ya wanajeshi wa Kenya waliouawa el-Ade bado haijulikani

Jeshi la Umoja wa Afrika nchini Somalia linakabiliwa na maswali mapya kutokana na shambulio katika kambi ya kijeshi ya Kenya mwezi uliopita.

Wanamgambo wa al-Shabab walidai kuwaua wanajeshi zaidi ya 100.

Jeshi la Kenya bado halijatoa idadi kamili ya wanajeshi waliouawa katika kambi hiyo ya al-Ade, kusini mwa Somalia na huenda likawa shambulio lililosababisha vifo vya wanajeshi wengi zaidi wa AU nchini Somalia.

Shambulia hilo, pamoja na vita vya hivi karibuni vya kudhibiti mji wa bandari wa Merca, ni ishara kwamba wanamgambo wa al-Shabab bado ni tishio licha ya wanajeshi wa AMISOM kuwa Somalia tangu 2007.

Umoja wa Mataifa uliunda kikosi hicho cha majeshi ya Afrika lengo kuu likiwa “kupunguza hatari kutoka kwa al-Shabab” na kusaidia serikali ya Somalia kudhibiti maeneo yote ya nchi hiyo.

Hata hivyo, hilo bado halijatimia.

Baada ya shambulio hilo la El Ade, majeshi ya AMISOM yalijiondoa kutoka kwa miji kadhaa kusini mwa Somalia katika kile ambacho maafisa wanasema ni hatua tu ya kijeshi.

Image caption Wanajeshi wa Amisom waliingia Somalia 2007

Maeneo haya ya kusini mwa Somalia inaaminika kwamba ni ngome ya al-Shabab na kuna uwezekano wameanza kuibuka tena.

Shambulio lililotekelezwa dhidi ya wanajeshi hao ambao wana jukumu la kulinda nchi ya Somalia lazima linawapa tumbojoto viongozi wakuu katika AU.

Hasara iliyokumba majeshi ya Kenya inafuatia mashambulizi ya aina hiyo dhidi ya majeshi ya muungano wa Afrika kutoka Uganda and Burundi mwaka uliopita.

Katika mkutano wa viongozi wan chi wanachama wa Umoja wa Afrika katika mji wa Addis Ababa, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitoa wito wa kutolewa kwa “usaidizi zaidi kwa wanajeshi walio Somalia”.

Wanajeshi walioko Somalia bila shaka watafurahia usaidizi zaidi lakini wamekuwa wakijaribu kujikakamua.

Haki miliki ya picha PSCU
Image caption Rais Kenyatta amesema Kenya haitaondoa majeshi yake Somalia

Katika ziara yake katika eneo la el-Ade baada ya shambulizi, kaimu kamanda mkuu wa Amisom Jenerali Nakibus Lakara alisisitiza kuhusu jukumu la wanajeshi hao.

“Amisom si jeshi la kulinda amani, ni jeshi la kivita," alisema.

“Na katika vita lazima kuwepo na majeruhi, la muhimu ni kwamba lazima tuhakikishe majeruhi upande wa Amisom ni wachache.”

Hata baada ya hasara, Rais Kenyatta amesisitiza kwamba taifa la Kenya halitatikisika na litaendelea na kampeni yake ya kijeshi nchini Somalia

Kuna baadhi ya watu kutoka Kenya wanaotaka majeshi kuondolewa nchini Somalia, lakini Rais Kenyatta anataka kuepukana na uwezekano wa kuacha pengo nchini Somalia ambalo linaweza kutumiwa na wanamgambo wa al-Shabab kujijenga na kuwa tishio tena kanda hii.

"Huu si wakati wa kuyumbayumba na kusikiza sauti za kushindwa na kukata tamaa," alisema.

Kuna wachanganuzi wanaoashiria kwamba hauwezi kuweka msingi wako wa sera za kigeni za nchi katika kujaribu kuonesha kwamba huna uoga.

Na pia, kuna maswali kuhusu sura ya baadaye ya vikosi vya AU nchini Somalia.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Al-Shabab wamefurushwa maeneo mengi lakini bado hutekeleza mashambulio mara kwa mara

Katika muda wa miaka tisa, Amisom imeweza kutwaa maeneo mengi na kuwafurusha wanamgambo wa al-Shabab kutoka baadhi ya maeneo, kusaidia serikali na kuhakikisha kuwepo kwa mazingira yanowezesha ukuaji wa kiuchumi, lakini haijaweza kukomesha mashambulio.

"Kuna umuhimu wa kuweka kigezo cha kupima mafanikio nchini Somalia,"anasema Abdullahi Boru, mchambuzi wa Masuala ya Usalama

"Nguvu za kijeshi hazitoshi," anasema, kuna pia umuhimu wa "kuwashawishi Wasomali wa kawaida kwamba harakati za jeshi hilo ni za kuwafaa”, la sivyo, "vita hivi havitakua na maana.”

Wanajeshi wa Amisom pia wanafaa kuwezesha serikali ya Somalia kupigana na al-Shabab kivyake "na kwa sasa hilo ni jambo ambalo halijafanyika”, anasema David Wagacha kutoka kituo cha kutoa ushauri cha Paradec.

Migawanyiko katika Amisom pia inafaa kuangaziwa.

Kwa sasa, Somalia imegawanywa katika sehemu tofauti, kila sehemu ikisimamiwa na jeshi kutoka nchi tofauti chini ya Amisom.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Al-Shabab wamewahi kushambulia kambi za wanajeshi wa Burundi na Uganda nchini Somalia

Hili limepelekea baadhi kuamini kuna ukosefu wa ushirikiano baina ya majeshi kutoka nchi husika.

Bw Wagacha anasema "licha ya hatua zilizopigwa katika kukomboa baadhi ya miji kutoka kwa al-Shabab, kunaonekana kutokuwa na ushirikiano baina ya mataifa yanayochangia wanajeshi Amisom, pamoja na kutoaminiana.

"Hivi vitaathiri uwiano pamoja na vita dhidi ya adui mmoja – al-Shabab.”

Utathmini wa kina unafaa kufanywa kabla ya kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuandaliwa kujadili majukumu ya Amisom.

Mabadiliko pia yanafaa kufanyika kuangazia udhaifu uliojitokeza wakati wa shambulio hilo la mwezi Januari.