'Waliotungua' helikopta TZ jela miaka 15

Gower
Image caption Gower alifariki baada ya ndege yake kudunguliwa

Watu wanne walioshtakiwa kuhusiana na kutunguliwa kwa helikopta iliyokuwa na rubani Mwingereza Roger Gower wamehukumiwa kufungwa jela miaka 15 kila mmoja.

Wanne hao, Njile Gunga, Shija Mjika, Dotto Pangani na Moses Mandagu, walihukumiwa katika mahakama ya wilaya ya Bariadi, mkoa wa Simiyu baada ya kukiri mashtaka.

Wamehukumiwa kwa makosa ya kumiliki na kupatikana na silaha kinyume cha sheria.

Gunga alikiri shtaka la ziada na kwa jumla atatumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Washtakiwa hao walikuwa wamekiri mashtaka hayo Jumatano lakini Hakimu Mfawidhi wa wilaya ya Bariadi Mary Mrio hakuweza kuwahukumu wakati huo kwa kuwa ushahidi dhidi yao haukuwa umewasilishwa wakati huo.

Njile Gunga bado anasubiri kesi nyingine mbili, moja ya mauaji ya rubani huyo na nyingine ya kuhujumu uchumi.

Kesi hizo zitatajwa katika Mahakama ya Mkoa wa Simiyu.

Rubani Gower alifariki baada ya helikopta yake kutunguliwa akishiriki operesheni ya kukabiliana na majangili katika pori la akiba la Maswa, wilayani Meatu.