Museveni kuhudhuria mdahalo wa wagombea Uganda

Museveni
Image caption Rais Museveni ameahidi kwamba atahudhuria

Wagombea wote wa urais nchini Uganda, akiwemo Rais Yoweri Museveni, wanatarajiwa kushiriki mdahalo wa pili wa kupeperushwa moja kwa moja kwenye runinga.

Uchaguzi mkuu unazidi kukaribia na sasa zimesalia siku tano tu.

Rais Museveni, ambaye alisusia mdahalo wa kwanza uliofanyika tarehe 15 Januari, anatarajiwa kushiriki mdahalo wa leo unaotarajiwa kuanza saa moja jioni.

Image caption Maandalizi yamekamilika

Katibu wake Meja Edith Nakalema amenukuliwa na gazeti la Daily Monitor la Uganda akisema ni kweli Bw Museveni atahudhuria.

"Rais ana haki ya kusema ‘ndio’ au ‘hapana’ kadiri anavyotaka,” Meja Nakalema amenukuliwa na gazeti hilo.

Wageni 1,500 wanatarajiwa kuhudhuria mdahalo wa leo ambao utafanyika katika ukumbi wa Victoria, hoteli ya Serena mjini Kampala.

Mdahalo huo umeandaliwa na Baraza la Dini Mbalimbali Uganda na Baraza la Wazee la Uganda.

Kiongozi wa maandalizi ya mdahalo huo, Jaji James Ogola, ambaye ni mwenyekiri wa baraza la wazee, amesema mdahalo wa leo utaangazia sera ya kigeni na mahusiano ya kimataifa nchini Uganda.

Vilevile wagombea watatakiwa kutoa mipango yao ya siku za usoni ya kuiongoza Uganda.‪

Uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 18 Februari umewavutia wagombea wanane wa urais.

Watakaokabiliana na Bw Museveni uchaguzini ni DKt Kizza Besigye, Bw Amama Mbabazi, Abed Bwanika, Maureen Kyalya, Meja (Mstaafu) Benon Biraro, Joseph Mabirizi na Venansius Baryamureeba.