Museveni ahudhuria mdahalo wa wagombea Uganda

Museveni Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Museveni amesema anayeungwa mkono na wananchi ndiye atakayeshinda

Rais Yoweri Museveni hatimaye amehudhuria mdahalo wa wagombea wa urais baada ya kususia mdahalo wa kwanza.

Mdahalo huo umefanyika katika hoteli ya Serena mjini Kampala.

Wagombea wengine walifurahia kufika kwa Bw Museveni na kusema walimkosa sana wakati wa mdahalo wa kwanza tarehe 15 Januari.

Mdahalo huo uliangazia sana sera ya kigeni ya wagombea hao na mipango yao ya siku za usoni za taifa la Uganda.

Aliwashukuru waandalizi wa mdahalo na kujitetea ni kwa nini hakuhudhuria mdahalo wa kwanza.

"Sikuja mara ya mwisho kwa sababu nilikuwa mbali, pia nilikwua pia na shaka kuhusu jinsi ungeendeshwa. Lakini si neno kwa sababu kulikuwa na runinga,” amesema akitoa hotuba yake ya kutanguliza katika mjadala.

"Nimefika hapa kuzungumza kuhusu Uganda, si mambo dhahania. Ukitaka dhahania na Tuzo ya Fasihi ya Nobeli au tuzo katika utunzi, basi unaweza kuzungumza utakavyo.”

"Nina furaha kwamba nimekuja hapa kuwazungumzia moja kwa moja. Wasiwasi wangu kuhusu jinsi ya kuendesha mjadala ni kwa sababu ya muda. Haya ni masuala mazito, si mambo ya shule. Lakini sasa niko hapa. Demokrasia ni rahisi, watu wasipokuunga mkono huwezi kushinda.”