Ehud Olmert aanza kifungo jela Israel

Ehud Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Olmert alikuwa waziri mkuu 2006-2009

Ehud Olmert ameanza kifungo cha miezi 19 gerezani, na kuweka historia ya kuwa waziri mkuu wa zamani wa Israel wa kwanza kukaa jela.

Olmert alihukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani mwaka wa 2014 baada ya kupatikana na kosa la ufisadi, wakati alipokuwa meya wa mji wa Jerusalem.

Kifungo hicho kilipunguzwa hadi miezi 18, Desemba mwaka uliopita, lakini kikaongezwa tena kwa mwezi mmoja baada ya kupatikana na hatia nyingine ya kujaribu kuficha ukweli.

Katika kanda ya video iliyotolewa mapema hii leo Olmert, mwenye umri wa miaka 70, amesema anapinga vikali tuhuma hizo za rushwa.

Kanda hiyo ilitolewa muda mfupi kabla ya Olmert, ambaye aluhudumu kama waziri mkuu kutoka mwaka wa 2006-2009, kuwasili katika gereza la Maasiyahu, iliyoko mjini Ramle.

Machi 2014, alipatikana na hatia ya kupokea rushwa ya dola 129,000, wakati alipokuwa meya wa Jerusalem, kutoka kwa mjenzi mmoja na Shekel 60,000 kutoka kwa mwingine.

Hata hivyo mahakama ilimuondolea kesi ya pili ya kupokea hongo nyingine ya Shekel 500,000, na hivyo kupunguza hukumu yake hadi miezi 18.